Monday 24 October 2016

Mamelodi Sundowns ndio vidume wapya wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika licha ya kufungwa na Zamalek1-0



Wachezaji na viongozi wa timu ya Mamelodi Sundowns wakishangilia na Kombe la Ligi ya Mabingwa wa Afrika walilolitwaa licha ya kufungwa bao 1-0 na Zamalek jana.

CAIRO, Misri
MAMELODI Sundowns imeweka historia mpya baada ya kutwaa kwa mara ya kwanza taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na Zamalek katika mchezo wa marudiano wa fainali uliofanyika Alexandria.

Timu hiyo ya Afrika Kusini ilitwaa taji hilo kwa kupata ushindi wa jumla ya mabao 3-1 baada ya kushinda 3-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wao kabla ya juzi kufungwa bao 1-0.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Afrika Kuisni kutwaa taji la Afrika, ambayo kwa mara ya mwisho ilitinga fainali mwaka 2001 wakati walipofungwa na wapinzani wakubwa wa Zamalek, Al Ahly.

Zamalek walipata bao hilo pekee katika dakika ya 62 lililofungwa na Stanley Ohawuchi licha ya kutawala mchezo huo na kufanya mashabulizi kibao langoni mwa Sundowns.

Lakini uzuiaji wa Sundows uliisaidia timu hiyo kuwabana wapinzani wao na kufaidika na ushindi mnono wa mabao 3-0 walioupata katika mchezo wa kwanza na kuwawezesha kutwaa ubingwa.

Zamalek iliingia uwanjani katika mchezo huo ikiwa na matumaini kibao ya kubadili matokeo hayo huku Bassem Morsi akiwasalimia wapenzi wa soka na kumshangilia kwa nguvu wakati mchezo huo ukianza.

Lakini walikuwa Sundowns ndio walikuwa wa kwanza kufanya shambulio la nguvu pake mshambuliaji wake Mzimbabwe Khama Billiat alipopiga shuti lilipaa juu ya lango la Zamalek katika dakika ya tano tangu kuanza kwa mchezo huo.

Zamalek nusura wapate bao la kuongoza katika dakika ya 12 wakati Ohawuchi, ambaye ndiye pekee aliyeongezwa katika kikosi hicho, alipenya kwa mabeki lakini alishindwa kufunga baada ya kupaisha mpira.

Sundowns ilipata pigo baada ya kipa wake namba moja Mganda Onyango alipolazimika kutoka uwanjani baada akiwa katika machela baada ya kuumua kifundo cha mguu, na kumuingia kipa wa akiba Wayne Sandilands katika dakika ya 28.

Lakini hakuwa na kazi ngumu hadi dakika 15 zilipopita pale ilipombidi kuokoa mchomo uliopigwa na nahodha wa Zamalek Ahmed Tawfik.

Zamalek waliongeza presha katikati ya kipindi cha kwanza lakini walikutana na kizingiti kikali kutoka kwa safu ya ulinzi kutoka kwa mabeki wa Sundowns na mara nyingi walijikuta wakimwaka pale walipojaribu kufanya shambulio la kushtukiza.

Billiat, Percy Tau na Anthony Laffor wote wangeweza kuifungia Sundowns baada ya kufanya shambulizi ya kushtukiza, hasa katika dakika nane za nyongeza za kipindi cha kwanza kufidia mpira kusimama ili kumpa matibabu Onyango.

Katika kipindi cha pili, mchezaji wa Zamalek, Ramzy Khaled alipiga mpira wa adhabu mara baada ya mapumziko kabla Ohawuchi hajapiga shuti nje ya eneo la penalti.




No comments:

Post a Comment