Sunday, 9 October 2016

Timu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) yapania kufanya makubwa katika mashindano ya Shimiwi Dodoma 2016
Timu ya Wavuta Kamba wa TAA wakijifua katika mazoezi jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) inaendelea na mazoezi makali kujifua kwa ajili ya mashindano ya Shirikisho ya Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi) yatakayofanyika Dodoma baadae mwezi huu.

TAA kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa katika mazoezi makali kujiandaa na mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika Dodoma kuanzia Oktoba 17 hadi 27 mwaka huu.
Timu ya Netiboli  ya  TAA ikifanya mazoezi kwenye uwanja wao jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA).
Timu hiyo inayotarajia kushiriki katika michezo ya netiboli, kuvuta kamba, soka, karata, bao, baiskeli na mingine, inajifua kwenye uwanja wao uliopo jirani kabisa na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Timu ya netiboli inanolewa na mchezaji wazamani wa timu ya bandari na taifa, Taifa Queens, Judith Ilunda huku soka na kuvuta kamba nazo zikinolewa na makocha wenye uwezo mkubwa.

Kocha wa timu ya kamba ni Abunu wakati yule wa soka ni Kingley.
Timu ya  Soka ikifanya vitu vyake katika mazoezi yao kujiandaa na Shimiwi.
Bonanza la Uzinduzi wa Mashindano ya Shimiwi lilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi) Septemba 10 na kuhudhuriwa na wizara na taasisi mbalimbali za Serikali hapa nchini.
Mchezaji wazamani wa timu ya Bandari na timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, Judith Ilunda (mwenye fulana nyekundu) akiongoza mazoezi ya timu ya TAA wakijiandaa kwa ajili ya Shimiwi.
Mashindano ya Shimiwi yanafanyika mkoani Dodoma ili kuunga mkono agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la Serikali kuhamia katika makao makuu ya nchi.

Kingine ni kuwapa nafasi watumishi wa umma ambao hawajawahi kufika Dodoma kufahamu mazingira pia kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya kuhamia.
 

No comments:

Post a Comment