Friday 14 October 2016

Watanzania wang'ara Dar Rotary Marathon 2016 huku wakivunja rekodi ya njia


Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi akifurahia jambo kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Dar Rotary Marathon 2016 katika viwanja vya The Green Oysterbay leo pamoja na maofisa wengine wa Bank M na Rotary Club.

Na Mwandishi Wetu
GABRIEL Gerald amevunja rekodi ya Dar Rotary Marathon wakati wanariadha wengine wa Tanzania wakitamba katika mbio hizo zilizofanyika jana na kuhudhuriwa na maelfu.

Mwanariadha huyo alimaliza mbio hizo kwa kutumia saa 1:01:49 wakati rekodi iliyopo ni ya saa 1:02, huku akiwapita wanariadha walioshiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil.
Wanariadha wa Tanzania, Felix Alphonce (kulia) na Dickson Marwa wakiteta kabla ya kuanza kwa mbio za kilometa 21 za Dar Rotary Marathon leo.
Alphonce Felix na Fabian Joseph walioshiriki Michezo ya Olimpiki 2016 walijikuta wakipigwa bao na Gerald ambaye alikosa sekunde nne tu kufuzu kwa Olimpiki katika mbio za meta 10,000, walipomaliza katika nafasi ya tatu na 12.

Mwanariadha mwingine wa Tanzania kwa upande wanaume walioshiriki Olimpiki, Said Makuka alikuwepo jana, lakini hakushiriki mbio hizo. Mshindi wa pili alikuwa Ismail Juma aliyetumia saa 1:01:52 huku Benard Msau na Peter Kipte wote wa Kenya wakimaliza wa nne na tano kwa kutumia saa 1:02:25 na 1:03:14.
 
 Kwa upande wa wanawake, Mnyarwanda Salome Nyirarukundo alifanikiwa kutetea ubingwa wake wa mwaka jana baada ya jana kumaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:11.34.68 huku Mtanzania Failuna Abdi akimaliza wa pili kwa saa 1:12:27 na Angela Daniel alimaliza wa tatu kwa saa 1:13:22:23 na Sara Ramadhani alimaliza wa nne kwa saa 1:14:34.23. 

Nyirarukundo ndiye mwanariadha bora wa Rwanda wa mwaka 2016 baada ya kuwapiku wenzake kwa mbali katika kura za uteuzi.

Alphonce, ambaye ni mshindi wa tano wa Olimpiki ya Rio katika marathon, alisema mbio zilikuwa ngumu hasa ukizingatia kuwa ndio kwanza ameanza mazoezi baada ya kuwa katika mapumziko kutokana na Michezo ya Olimpiki.

Alisema siku zote mshindi ni yule aliyejiandaa vizuri na alimpongeza Gerald kwa ushindi huo na alisema ndio ameanza mazoezi kwa mashindano mbalimbali.
 
Mshindi wa mbio hizo, Gerald alisema mbio zilikuwa nzuri na zenye ushindani wa hali ya juu na alishinda kwa sababu alijiandaa vizuri.

Nyirarukundo alisema mbio zilikuwa nzuri na alishinda kwani ndio kwanza alirejea kutoka katika Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, ambako alishiriki mbio za meta 10,000.
Mbio hizo ziliongozwa na rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alishiriki matembezi ya kilometa tano na baadaye alitoa zawadi kwa washindi.
 
Mwinyi alisema kuwa mbio hizo zinazidi kukua na kuwapongeza waandaaji kufanikisha mbio hizo za tisa tangu kuanza kwake.
 
 
 

 

 


 
 

 




 

 

No comments:

Post a Comment