Wednesday 26 October 2016

Serikali yazipiga stop Yanga, Simba kuendelea na michakato ya kubadili umiliki wa klabu hizo



Kaimu Katibu Mkuu wa Barraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja (kulia) akimkabidhi zawadi kocha mkuu wa timu ya taifa ya riadha iliyoshiriki Michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, Francis John. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Riadha Tanzania (RT), Rehema Killo na aliyekuwa kiongozi wa msafara wwa timu ya Tanzania ya Olimpiki, Suleiman Jabir. 

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezipiga stop Yanga na Simba kuendelea na michakato yao ya kubadili umiliki wa klabu hizo hadi pale yatakapofanyika marekebisho ya katiba zao.

Hayo yalitangazwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed kiganja wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Kiganja alisema kuwa Serikali haikatai mabadiliko ya uendeshaji katika klabu hizo pamoja na zingine za wanachama, ila inachotaka kwanza kufanyike marekebisho ya katiba zao, ambayo sasa hayaruhusu mabadiliko hayo.

Alisema kuwa BMT inapenda kuona kwamba wahusika wanafuata sheria na taratibu za nchi katika kufikia malengo yao, ambapo alisisitiza kuwa kuendelea na michakato hiyo kabla ya kurekebisha katiba zao ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Hivi karubuni kumeibuka michakato ya watu wakitaka kubadilisha umiliki wa klabu za wanachama na kuzielekeza katika utaratibu wa hisa na ukodishwaji, vitendo vimesababisha migogoro mikubwa ambayo inaashiria uvunjifu wa amani…”

Kiganja alisema tayari mezani kwake kuna barua kibao za wanachama wa Yanga wanaopinga vikali kuendelea kwa mchakato huo wa kubadilisha umiliki.

Ibara ya 56 ya Katiba ya Yanga iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 inaeleza kuhusu kampuni ya umma:

Inaeleza kuwa kutakuwa na kampuni itakayojulikana kama Young African Sports Corporation Limited ambayo itasajiliwa chini ya sheria ya makampuni kama kampuni ya umma yenye hisa.

Sehemu ya pili ya ibara hiyo inasema wanachama wote katika klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya Katiba ya mwaka 2007 wako hai watakuwa,kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakapopata kwa mujibu wa muafaka wa Yanga uliofikiwa na Wana Yanga Juni 22, 2006.

Klabu itamiliki hisa zilizosawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika klabu hiyo.

Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili, ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.

Tayari Yanga iko chini ya Kampuni ya Yanga Yetu ambayo ni mali ya mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuf Manji, ikiwa ni kinyume na katiba yao wenyewe.

Kiganja alisisitiza kuwa klabu zisitishe mipango ya kubadilisha uendeshaji na ziendelee kuwa mali ya wanachama.
Wakati Yanga walikuwa tayari wameishaingia mkataba wa miaka 10 wa kuikodisha klabu yao, wenzao wa Simba walijipa miezi sita kukamilisha taratibu za kuuza hiza.

No comments:

Post a Comment