Sunday 29 October 2017

Wafanyakazi TAA kupatiwa mafunzo ya kazi

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.Richard Mayongela (wa tatu kulia), jana akiandika mambo mbalimbali katika mkutano na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza. Wa pili kushoto ni Meneja wa kiwanja hicho Bi. Esther Madale na wa kwanza kulia ni Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Agustino Magele.


Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wataendelezwa kwa kupata mafunzo mbalimbali, ili kuongeza weledi na tija kazini, imeelezwa.

Kauli hiyo ambayo ni moja ya malengo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela jana alipoongea na wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Mwanza pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.

Bw. Mayongela alisema  wafanyakazi wakipata mafunzo zaidi ya kazi zao wataisaidia serikari kufanikisha moja ya malengo yake makuu ya kukuza uchumi, ambapo watakuwa na mbinu za kisasa zikiwemo za ukusanyaji wa mapato kwa uaminifu na uadilifu, ambapo viwanja vya ndege ni moja ya vyanzo vya mapato hayo.

Hata hivyo, alisema  atapitia majalada ya wafanyakazi wote ili kubaini waliojiendeleza kwa mafunzo mbalimbali, lakini wanafanyakazi zisizo za kada zao,  hivyo ataangalia uwezekano wa kuhamishiwa kwenye kada zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Edger Mwankuga aliyesimama jana akiwasilisha hoja zake mbalimbali mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (hayupo pichani) alipokutana na wafanyakazi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

“Wapo wafanyakazi wa kada mbalimbali waliojiendeleza, lakini hadi sasa bado wapo kwenye kada walizoajiriwa nazo na zipo tofauti na sasa, nitangalia uwezekano wa kupangiwa kada zao ili waweze kuenda na kasi ya kazi zinazowahusu,” alisema Bw.Mayongela.

Pia malengo yake mengine alisema atahakikisha anaboresha maslahi ya wafanyakazi wa ngazi ya chini ili kunyanyua ari na tija kazini, ambapo kwa sasa wamekata tamaa kutokana na maslahi duni yasiyolingana na kazi zao.

Lakini aliwaasa wafanyakazi wenye mamlaka ya kuingia mikataba na wafanyabiashara, kubadilika na kuhakikisha wanatumia vyema sheria zinazowaruhusu kuingia mkataba baina yao na sio kukiuka, kwani inaweza kuwaletea matatizo, endapo itabainika kuwepo kwa udanganyifu uliosababisha upotevu wa mapato ya serikali, kwa kuwa atahakikisha TAA inajitosheleza kimapato na kujiendesha kwa baadhi  ya mambo ya ndani bila kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.

Alisema kwa sasa TAA imekuwa ikinyooshewa kidole kwa kusemwa vibaya na wadau mbalimbali, lakini  kupitia umoja na mshikamano wa wafanyakazi atahakikisha anarudisha taswira nzuri iliyokuwepo na kujenga Mamlaka mpya yenye kuaminika.

Pia alizungumzia uadilifu na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi, kuacha mara moja vitendo vinavyoweza kuhujumu jitihada na vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/18 hadi kufikia 2020/21.


Wafanyakazi wa idara mbalimbali za kiwanja cha ndege cha Mwanza na kikosi cha zimamoto na uokoaji, wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela alipokutana nao jana kujadili masuala mbalimbali ya kiuendeshaji.

“Mimi ni mgeni katika nafasi hii (ya Ukurugenzi), lakini ninachoomba tufanye kazi kwa bidii, mvunje makundi na tukosoane kwa kujenga na sio kubomoa, na viongozi muache kupendelea mtende haki kwa wafanyakazi wote, tukiwa na lengo la kuijenga TAA yenye mwelekeo mpya,”alisema Bw. Mayongela.

No comments:

Post a Comment