Monday 30 October 2017

Kivumbi mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kesho

Baadhi ya wachezaji wa Basel ya Uswisi wakifanya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi kesho Jumanne.

ZURICH, Uswisi

RAUNDI ya nne ya Ligi ya Mabigwa wa Ulaya hatua ya makundi inaendelea tena kesho, huku Bayern Munich, Chelsea, Manchester United, Barcelona na Atletico Madrid ni miongoni mwa timu zitakazoshuka dimbani.

Tayari kila timu imeshacheza mechi tatu na leo na kesho zinakamiisha mechi nne kila moja na kubakisha mbili ili kukamilisha hatua ya makundi kabla ya kufuzu kwa 16 bora au hatua ya kwanza ya mtoano.

Timu mbili za kwanza kutoka katika kila kundi zitakuwa zimefuzu kucheza hatua hiyo ya timu 16 bora.

BAYERN MUNICH

Bayern Munich wanatarajia kukabiliana na Celtic iliyo tofauti kabisa katika mchezo wa Kundi B utakaofanyika leo jijini Glasgow tofauti na kikosi walichocheza nacho awali, ambacho walikifunga mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza Ujerumani.

Mshambuliaji Leigh Griffiths anasema kuwa Celtic kwa sasa wako vizuri zaidi na mabingwa hao wa Ujerumani wasitarajie kupata mteremko.

 

Kimsimamo, Celtic wako katika nafasi ya tatu katika Kundi B, lakini sasa imefikia rekodi yao waliyoiweka miaka 100 iliyopita ya kucheza mechi 62 za nyumbani bila kufungwa.

Timu hiyo inajua kuwa itakuwa nje ya mashindano hayo endapo itapoteza mchezo huo na Paris St-Germain (PSG) itakwepa kipigo cha nyumbani kutoka kwa Anderlecht.

"Mchezo utakuwa tofauti kabisa hapa, hasa kutokana na mashabiki kuwa nyuma yetu, “ alisema Griffiths.

"Katika kipindi cha pili [mchezo wa ugenini] tulicheza vizuri zaidi. Tulitengeneza nafasi kibao za kufunga mabao.

Endapo kikosi cha kocha Brendan Rodgers kitatolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa leo, watabaki kusaka nafasi ya tatu ili kufuzu kucheza Ligi ya Ulaya katika mechi mbili za mwisho hatua ya makundi.

Rodgers alikuwa kocha wa Liverpool F.C. kuanzia mwaka 2012 hadi 2015 kabla ya kutua Celtic, hivyo leo atakuwa akipambana na timu yake yazamani.

Nyumbani, Celtic inaoongoza katika Ligi Kuu ya Scotland, lakini Griffiths anasema kuwa walikatishwa tamaa kupoteza pointi mbili Jumamosi baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Kilmarnock.

 

Wakati winga Patrick Roberts ataukosa mchezo huo dhidi ya mabingwa hao wa Ujerumani kutokana na maumivu, kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes ana uhakika Robert Lewandowski atakuwa fiti kwa mchezo huo.

Wakati huohuo, beki wa kulia wa Ujerumani Joshua Kimmich anategemea timu yao itafuzu kwa hatua ya 16 bora huku ikiwa imebakisha mechi mbili kabla ya kukamilisha hatua ya makundi wakati watakaposafiri kwenda Glasgow.

CHELSEA DIMBANI

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte anasema kuwa anatumaini ataweza kumchagua kiungo N'Golo Kante kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Roma utakaofanyika leo.

Kante aliumia nyama za paja wakati akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa mapema mwezi huu na alikosa mechi tano za awali za Chelsea, ikiwemo ile waliotoka sare ya 3-3 nyumbani dhidi ya Roma siku 11 zilizopita.

Kimsimamo Chelsea inaongoza katika Kundi C ikiwa na pointi saba na inaweza kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya 16 bora endapo itapata ushindi katika mchezo wake huo wa Italia leo.

Kocha Conte anasema kuwa hawezi kuthubutu kumchezesha Kante endapo mchezaji huyo Mfaransa hatakuwa fiti vya kutosha.

"Yeye (Kante) anaweza kuwa tayari," alisema kocha huyo Muitalia wakati alipozungumza na waandishi wa habari. Najua sana umuhimu wa mchezaji huyu. Nataka kuhakikisha kuwa yuko tayari….”

Sare na Roma katika Uwanja wa Stamford Bridge ilikuja baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kufungwa mfululizo na kuwaacha wakiwa pointi tisa tofauti na vinara Manchester City.

Hatahivyo, ushindi wa timu hiyo katika ligi dhidi ya Watford na ule wa Bournemouth na kuifunga Everton katika Kombe la Ligi, kumeiongezea nguvu timu hiyo.

"Ulikuwa ushindi mzuri (1-0 dhidi ya Bournemouth Jumamosi) kwa kujijengea kujiamini, ushindi mzuri kabla ya mchezo mwingine mgumu dhidi ya Roma katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, “alisema.

"Ushindi ulikuwa muhimu kutupa mwendelezo kushinda dhidi ya Watford, na Everton katika (Kombe la Ligi), na sasa tunajiandaa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Roma.”

Alvaro Morata anatarajia kuanza katika mchezo huo wa leo, licha ya kutofunga katika mechi nne tangu aliporejea kutoka katika maumivu ya nyama za paja aliyoyapata walipocheza na kufungwa na Manchester City mwezi uliopita.

 

VINARA BARCELONA

Barcelona wenyewe leo watakuwa dimbani kupepetana na Olympiakos Piraeus katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi.

Barcelona ambao wanashuka uwanjani leo huku wakiwa wanaoongoza katika kundi lao kwa kuwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu hadi sasa.

Mbali na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Barcelona pia inaongoza katika Ligi Kuu ya Hispania ya La Liga ikiwa pointi nne dhidi ya Valencia iliyopo katika nafasi ya pili.

 

MANCHESTER UNITED

Manchester United leo wanashuka dimbani kucheza dhidi ya Benfica katika mchezo itakaofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford ikiwa imeshinda mechi zake zote tatu na kujikusanyia pointi tisa.

Katika ligi ya nyumbani, Manchester United iko katika nafasi nzuri kwani iko nyuma ya vinara wa Ligi Kuu ya England Man City.

MECHI ZINGINE LEO

Leo Oktoba 30 mechi zingine zitakazofanyika ni ile ya Atlético Madrid itakayokuwa mwenyeji wa Qarabağ katika mchezo utakaofanyikia kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano, Sporting CP     itaikaribisha Juventus katika mchezo mwingine.

Nayo Basel itakwaana na CSKA Moskva         katika mchezo mwingine wa mashindano hayo huku PSG watatoana jasho na Anderlecht katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Parc des Princes.

No comments:

Post a Comment