Monday, 23 October 2017

Lulu akana kusababisha kifo cha Steven Kanumba


Na Mwandishi Wetu

MUIGIZAJI wa Filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa hakusababisha kifo cha mpenzi wake Steven Kanumba na badala yake yeye ndiye angeuawa baada ya kupigwa na panga.

Lulu ambaye amebainisha wazi kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa miezi minne na Kanumba, alikuwa akienda mara kwa mara nyumbani kwake na kwamba walikuwa wanaficha mahusiano yao ili kukwepa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Akiongozwa na Wakili wake, Peter Kibatala, Lulu alidai mbele ya  Jaji Sam Rumanyika kuwa Aprili 6, 2012 alikuwa nyumbani kwao Tabata na jioni alitaka kwenda kwa marafiki zake Mikocheni kwa ajili ya kwenda klabu.

Alidai walikuwa wakiwasiliana na marehemu Kanumba kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi licha ya kwamba hakutaka kumwambia kama anataka kutoka na marafiki zake kwa sababu alikuwa hapendi atoke.

"Marehemu alikuwa akinipigia simu mara nyingi kujua nipo wapi ndipo nilimwambia kuwa nataka kutoka ili asinisumbue nikamueleza kuwa nitapita nyumbani kwake kumuaga, lakini sitokaa sana. Kabla ya kufika alinipigia na kunambia kuwa ataacha mlango wazi hivyo nipite mpaka chumbani..nyumba niliizoea hata asipokuwepo nilikuwa naenda," alidai Lulu.

Aliendelea kudai kuwa alimkuta Kanumba chumbani akiwa na taulo huku akipaka mafuta kichwani, ambapo yeye alikaa kitandani na kusalimiana.

"Kama tunavyojua marehemu alikuwa anajipenda sana hivyo alikuwa ameweka superblack kwenye nywele zake na kwamba alikuwa na mafuta maalum ili zing'ae. Tulisalimiana na muda kidogo simu yake iliita na alipokea alikuwa ni Chaz Baba  akamwambia anakuja. Wakati huo alikuwa anakunywa pombe aina ya Jack Daniel na Sprite na ameshaanza kulewa," alidai.

Pia alieleza kwa kuwa marehemu Kanumba alikuwa hapendi atoke, alimtaka waende sehemu moja ambapo mara nyingi akilewa huwa  anampiga hivyo hakutaka kumbishia kutoka naye.

Lulu alidai hupendelea kwenda disco wakati marehemu Kanumba alikuwa anapenda kwenda kwenye bendi ambazo alidai kwake  ni za kizee wakati huo aliwaahidi marafiki zake kuwa atarudi.

Alidai baadae marafiki zake walianza kumpigia kumuuliza ulipo ambapo aliogopa kupokea simu mbele ya Kanumba kukwepa kuulizwa  anakwenda wapi, hivyo alimuaga na kumueleza kuwa anakwenda kuchukua maji jikoni na alipofika kwenye korido  Kanumba alimfuatilia kwa nyuma na kumuuliza anaongea na nani.

"Nilijua utani huku nikiwa nacheka nikamjibu kuwa naongea na rafiki yangu kwa sababu nilizoea anapenda kujua naongea na nani  lakini baadae nilianza kuogopa baada ya kuona sura yake imebadilika hivyo nikawa natoka nje naye alianza kunifuata na hii sio mara ya kwanza kunipiga na hufanya hivi akiwa amelewa maana hata mtu alinipigia au kumkumbatia alikuwa hapendi," alieleza na kuongeza;

"Nilikimbia hadi nje wakati huo marehemu alikuwa na taulo hivyo nikadhani kwamba ataona aibu kutoka nje hivyo huku akiwa kifua wazi lakini alinifuata hadi nje umbali wa hatua 28 lakini aliendelea kunikimbiza hadi getini akatoka nje ya geti ambapo kuna barabara ya Sinza Kijiweni na Tandale..tuliendelea kukimbizana hadi nikajificha lakini aliniona na kunipiga vibao na kunifunga mikono yangu kwa mkono wake mmoja."

Muigizaji huyo pia alidai Kanumba alianza kumpiga mateke na kumburuza huku akiwa na taulo lake na kwamba mdogo wake, Seth Bosco alikuwepo lakini hakutoka kumsaidia.

Alidai baada ya kuburuzwa alinyanyuka na alipelekwa moja kwa moja hadi chumbani na mlango ulifungwa kwa funguo kwa ndani na kutupwa kitandani kwa sababu alihisi simu aliyokuwa anaongea naye ni mwanaume mwingine.

Lulu alidai marehemu Kanumba alitoa panga na kwa sababu walikimbia alikuwa anahema sana na kumwambia kuwa atamuua hivyo alianza kumpiga kwa mabapa ya panga kwenye mapaja naye alikuwa akikinga asikatwe usoni.

Vile vile, alidai  Kanumba alikuwa anapumua kwa kasi na kutupa panga chini na kuwa kama mtu anayekabwa baadae alinguka na kujigonga kwenye ukuta muda huo yeye alikuwa kitandani.

"Alipokuwa anataka kuamka nilihisi anataka kunifuata tena nikitoka nikajifungia chooni wakati huo yeye   alianza kutapatapa. Nilijaribu kupiga kelele kupata msaada lakini hakuna, baadaye nilisikia kishindo cha mtu kuanguka au mlango uliobamizwa na kusikia ukimya.

Sikujuwa za kama ameanguka nilihisi hasira zake tu kwani nilipofungua mlango  wa bafuni nilimkuta amelala na wakati huo kulikuwa na mwanga wa mshumaa kwani umeme ulikatika," alidai.

Lulu alidai kwa akili zake aliwaza kuwa Kanumba alijifanyisha kuzimia ili isiwe tatizo kwake ambapo alianza kumwambia kuwa hata mtu akija atamwambia kila kitu kilichotokea lakini akawa hajibiwi.

Alidai alichukua maji chooni na kumgusisha machoni kuona kama ataamka na baadaye alifungua mlango na kumuita Seth na kumueleza kuwa Kanumba ameanguka ambaye naye alijaribu kumuamsha lakini hakuamka na kumpigia simu daktari wake.

Lulu anasimulia kuwa alimwambia Seth hawezi kubaki nyumbani hapo badala yake akitoa naye atatoka kwani akiamka atamuua  hivyo aliondoka na gari hadi Coco Beach.

Aliendelea kudai kuwa alimpigia simu daktari wa familia Paplas  ambaye alikuwa anajua mahusiano yao na wakati akiumwa alikuwa anamtibu na kwamba alimueleza kuwa rafiki yake amempiga sana na iwe mara ya mwisho kumtafuta kwa sababu alimshikia panga na siku nyingine atamuua.

Alieleza kuwa alikuwa haruhusiwi kutoka nyumbani kwao usiku hivyo alikuwa anabeba nguo za ziada na anaporudi nyumbani asubuhi hudanganya kama alitoka kuosha vyombo wakati anatokea klabu.

"Nilipokea simu nyingi kuniuliza kama kweli Kanumba amekufa nilimpigia simu Seth, ambapo alikuwa hapokei nilimpigia Dk Paplas nikamuuliza kuhusu masuala ya nyumbani imekuwaje kwa sababu amepigiwa simu kuuliza naye akamwambia kuwa hajafa ila wapo hospitali na kukata simu. Baadaye Dk Paplas alinipigia kuniuliza niko wapi tukutane," alidai

"Kwa sababu nilijua Kanumba na huyu daktari ni marafiki, nilijua anamtumia rafiki yake waweze kukutana tena  mara ya kwanza nilimkatalia na nikamuuliza kama amezidiwa yupo hospitali gani niende. Nilitaka anihakikishie alipo na asije na Kanumba na wala hakunambia kama ameshakufa," alieleza Lulu.

Alidai walikutana Bamaga na Dk Paplas na ndipo askari walimkamata bila ya kumwambia sababu na walipofika Kituo cha Polisi, Oysterbay Polisi akakutana na watu wengi akiwemo msanii Vincent Kigosi 'Ray' na kuhisi kwamba Kanumba amekamatwa.

Alidai alichukuliwa maelezo na kuonesha sehemu alizojeruhiwa kwa kipigo na askari wa kike ndiye aliyethibitisha na kwamba alichukuliwa maelezo mara nne ambapo alipata taarifa za kifo cha Kanumba akiwa selo.

Siku inayofuata, Lulu alidai alimueleza Afande Ernatus kwamba anaumwa hivyo alipelekwa hospitali ya Mwananyamala akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuandikiwa dawa.

"Sijasababisha kifo chake yeye ndiyo alikuwa ananishambulia kwa silaha pengine asingeanguka mimi ndio ningekuwa marehemu kwa sababu sikuwa na njia yoyote ya kujitetea kwa sababu ya umbile langu dogo," alidai Lulu.

Hata hivyo, Jaji Rumanyika alimtaka Lulu kueleza kama wakati huo anaendesha gari alikuwa na leseni, ambapo alidai kuwa hakuwa nayo mpaka baada ya matatizo hayo ndio aliomba leseni.


Kesi hiyo imeahirishwa mpaka leo ambapo upande wa utetezi utakuwa na shahidi mmoja Josephine Mushumbus ambaye wanadai kuwa yupo nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment