Monday 23 October 2017

TFF yatangaza kuziona Yanga, Simba ni sh 10,000

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru kuwa ni sh. 10,000 majukwaa ya mzunguko wakati jukwaa kuu ni sh. 20,000.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa utaratibu maalum umewekwa kuhakikisha idadi inayotakiwa ya watu 22,000 ndiyo wanaoingia uwanjani.

Alisema  mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, kwa kuwa uwanja mkubwa wa Taifa upo kwenye ukarabati.

Katika hatua nyingine, Lucas alisema Kamati mpya ya Uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) ya TFF itafanya kikao chake cha kwanza mjini Dar es Salaam, Alhamis ya wiki hii na kubwa likiwa ni maandalizi ya mchezo huo.

Alisema  ajenda nyingine katika kikao hicho ni kuteua Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi na Kamati nyingine mbalimbali.


Hiyo ni baada ya uchaguzi wa TPLB uliofanyika Jumapili Oktoba 15 mwaka huu na kupata uongozi mpya chini ya mwenyekiti wake Clement Sanga na makamu wake Shani Mlingo. Wajumbe ni Hamisi Madaki, Ramadhani Mahano, Almasi Kasongo na Edgar Chibura.

No comments:

Post a Comment