Sunday 1 October 2017

Pakacha Group laendesha kongamano la kujadili utatuzi wa changamoto za maji Kwembe, Kibamba, Msigani

Viongozi wa asasi ya Pakacha Group wakiwa na viongozi wa Kata ya Kwembe wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam kabla ya kongamano la kujadili changamoto zinazokabili maji katika kata hiyo jana.

Na Mwandishi Wetu

DIWANI wa Kata ya Kwembe wilayani Ubungo, Dweza Kolimba amesema asasi za kiraia zina nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika jamii kwa kushirikiana na wananchi na watendaji wa serikali.

Akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na asasi ya Pakacha Group kwa wananchi wa kata hiyo kwa ajili ya kujadili utatuzi wa changamoto ya maji, kuanzia ufuatiliaji wa rasilimali fedha na utekelezaji wake, Kolimba alisema asasi hiyo itasaidia kufanya watendaji na wananchi kufanya kazi kwa pamoja.

Alisema ushirikiano huo utasaidia kuibua changamoto zinazokwamishwa na rasilimali fedha au kutowajibika kwa baadhi ya watendaji.

Alisema asasi zinaweza kuleta mabadiliko kwa kufuatilia miradi ya maji, ambayo inakwamishwa kwa sababu mbalimbali na kuwaelimisha wananchi jinsi ya kulinda miundo mbinu ya maji na ufuatiliaji wake.

"Pia zinasaidia kutoa msukumo kwa utelekezaji wa miradi kwa kuibua hoja kwa wananchi, kwa lengo moja tu, kuleta maendeleo na sio malumbano yasiyo na msingi”, alisema mheshimiwa Kolimba.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kwembe, Hamisi Moto alisema kuwa jitihada zinafanyika ile kuondoa adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Kongamano hilo limefanyika kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kufuatilia fedha zinazotengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma ya Maji katika kata tatu za Kwembe, Kibamba na Msigani.

Diwani huyo alisema wananchi wanaweza kufanya ufuatiliaji kupitia mfumo wa Pets ukiwa na malengo ya kuboresha huduma za kijamii, kuhakiki utendaji wa serikali za mitaa na kuwezesha uandaaji wa mipango shirikishi.

Pets ni mfumo unaowezesha ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zinazotoka Serikali Kuu au halmashauri kwa maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi za mitaa hadi kata na kuendelea.

Verisiyus Magoti, mwakilishi wa mhandisi wa maji kutoka Manispaa ya Ubungo alisema wananchi washirikiane na watendaji ili kutatua kero za maji na jitihada zinaendelea kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana wakati wote.

Haroun Jongo, katibu wa Pakacha Group alisema kongamano hilo ni moja kati ya matatu yatakayofanyika katika Kata za Kibamba, Kwembe na Msigano kwa siku tofauti tofauti.


Alisema makongamano hayo hayana lengo la kuwagombanisha wananchi na viongozi, bali yanaweka msukumo katika kuhakikisha miradi inasimamiwa vizuri na inatekelezwa.








No comments:

Post a Comment