Monday 23 October 2017

Al Ahly yaichapa Etoile sasa kucheza fainali Ligi ya Mabingwa wa Afrika 2017 na Wydad Casablanca

CAIRO, Misri

KLABU ya Misri ya Al Ahly (pichani) sasa itakutana na Wydad Casablanca ya Morocco katika fainali ya mwaka huu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kuichapa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa mabao 6-2.

Kwa ushindi huo, Al Ahly imetinga fainali baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 7-4 katika mechi mbili za nusu fainali.

Katika mchezo wa marudio wa nusu fainali uliofanyika jijini Alexandria, Al Ahly ilionekana kuizidi kabisa safu ya ulinzi ya wapinzani wao hao wa Tunisia wakati wakikata tiketi hiyo ya kucheza fainali ikiwa ni mara yao ya 11.

Baada ya Ali Maaloul kufunga bao la kwanza kwa wenyeji dakika mbili baada ya kuanza mchezo huo, Walid Azarou alifunga bao la pili na kuifanya Etoile kutoka kabisa nje ya mchezo.

Bao la kujifunga lililofungwa na Rami Rabiaa liliipeleka Al Ahly katika fainali ya kwanza tangu mwaka 2013, huku Etoile ikijibu kupitia kwa Rami El Bedwi na Ihab Msakni kwa maba waliyofunga baadae.

 

Miaka minne iliyopita, Al Ahly iliifunga timu ya Afrika Kusini ya Orlando Pirates katika fainali wakati walipofanikiwa kutetea taji lao waliloshinda miezi 12 iliyotangulia.

Mchezo huo wa Jumapili ulipigwa mbele ya karibu mashabiki 40,000 jijini Alexandria, ambao walisaidia kuiongezea nguvu Al Ahly baada ya mechi nyingi za Misri kuchezwa bila ya mashabiki kutokana na sababu za kiusalama.

Kikosi cha kocha Hossam El Badry sasa kitakutana na Wydad katika mechi mbili za fainali, baada ya Wamorocco hao kuwafunga USM Alger ya Algeria kwa mabao 3-1 katia mchezo uliofanyika Jumamosi.

Wakati huohuo, Ahly sasa wanaweza kuongeza rekodi yao ya kutwaa taji hilo mara nane na hadi kufikia mara tisa endapo watafanikiwa kuifunga Wydad.

Mchezo wa kwanza wa fainali utafanyika wikiendi ijayo huku ule wa marudiano unatarajia kufanyika Novemba 3-5.


Timu yoyote itakayoshinda italiwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Fifa ya Kombe la Dunia kwa klabu yatakayofanyika Japan Desemba.

No comments:

Post a Comment