Sunday 1 October 2017

Chaneta waibuka na mikakati ya kuinua netiboli

Na Mwandishi Wetu

UONGOZI mpya wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) umesema kuwa umejipanga kuhakikisha unaleta maendeleo ya mchezo huo hapa nchini.

Akizungumza jana Katibu Mkuu mpya wa Chaneta, Judith Ilunda (pichani) alisema kuwa, wanajua changamoto zilizopo katika chama hicho, lakini wamejipanga kukabiliana nazo ili kuleta maendeleo katika mchezo huo.

Ilunda ambaye ni mchezaji wazamani wa timu ya Bandari Dar na timu ya taifa ya netiboli kwa muda mrefu, alisema kuwa watahakikisha mchezo huo unachezwa katika shule za msingi, sekondari na mitaani.

Alisema pia watahakikisha wanaendesha mashindano ya mara kwa mara na timu zenye ubora zinashiriki, ili kuhakikisha mchezo huo unarudi katika chati kama zamani kitaifa na kimataifa.

Alisema kamati yao mpya itakutana hivi karibuni mara baada ya kukabidhiwa ofisi na uongozi uliopita na kutangaza zaidi mipango yao ya muda mrefu na mfupi.

Uchaguzi Mkuu wa Chaneta ulifanyika mjini Dodoma juzi, ambapo Dk Devetha Marwa  aliutwaa uenyekiti baada ya kupata kura 53 dhidi ya Damian Chonya aliyepata kura nne.

Makamu ni Anna Gidaria aliyepata kuta 44 dhidi ya Winfrida Emmanue kura 10 na Pili Mogella alipata kura tatu.

Nafasi ya Katibu Mkuu ilikwenda kwa Ilunda aliyepata kura 50 dhidi ya makamu mwenyekiti aliyepita Zainabu Mbiri aliyeambulia kura sita, huku katibu msaidizi ni Hilda Mwakatobe aliyepata kura 30 dhidi ya 26 za Mwajuma Kisengo.

Nafasi ya mhazini haijajazwa baada ya mgombea pekee, Grace Khatibu kupata kura nne za ndio na hapana 49 na hivyo kutoweza kuchaguliwa kwa kuwa alikuwana kura nyingi za hapana.


Wapiga kura walikuwa 57 kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment