Saturday, 1 July 2017

Mjomba Mpoto atangaza utalii wa ndani Saba Saba

Msanii mahiri wa mashairi, Mrisho Mpoto au Mjomba akizungumza katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro katika Maonesho ya 41 ya Biashara ya Saba Saba jijini Dar es Salaam leo.
Na Mwandihsi Wetu
MRISHO Mpoto au Mjomba kama anavyojulikana sana na wapenzi wa sanaa nchini, leo alikuwa kivutio katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro katika maonesho ya 41 ya Biashara ya Saba Saba jijini Dar es Salaam.

Mjomba anayetamba kwa uimbaji mashahiri alivuta watazamaji kibao katika banda hilo, ambalo ni sehemu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuvaa mfano wa mnyama tembo.
Mjomba akiwa na Stara Thomas katika banda la Hifadhi ya Ngorongoro leo.
`Sanamu’ hiyo aliyoivaa kuanzia shingoni ina mfano wa masikio makubwa na pembe kama za ndovu pamoja na mkonga wake, ambavyo vilikuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi.

Mjomba pia alicheza ngoma za asili na baadae kuimba kibao chake cha Mjomba, akiongwa na bendi yake ya Mjomba iliyokuwa na wanamuziki kibao.

Wasanii wa Mjomba Band wakifanya vitu vyao leo.
Akizungumza katika viwanja hivyo, Mpoto alisema kuwa baadhi ya majukumu yake katika Ubalozi wa Ngorongoro ni kuelimisha na kuwahimiza Watanzania kufanya utalii wa ndani.

Alisema kila siku atakuwa katika banda hilo la Ngorongoro kutoa elimu na kuwashawishi watu kujua faida za utalii wa ndani na kutembelea vivutio.
Mjomba alivitaja baadhi ya vivutio hivyo katika Bonde la Ngorongoro ni pamoja na mchanga unaotembea, watu kuishi na wanyama wakali, nyayo za mtu anayesemekana ni wa zamani kabisa duniani.

Alisema ni aibu kubwa kuona watu kutoka nje ya Tanzania waijua Ngorongoro na vivutio vyake, kuliko Watanzania wenye nchi yao.
Naibu Muhifadhi wa Ngorongoro, Asangue Bangu (kushoto) akihojiwa na Mtangazaji Pascal Mayala katika banda hilo la Ngorongoro leo jijini Dar es Salaam.
Naye naibu mhifadhi wa Bonde la Ngorongoro, Asangue Bagu alisema Mpoto atawasaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utalii wa ndani.

No comments:

Post a Comment