Sunday 16 July 2017

Watu Nane wauawa uwanjani nchini Senegal

DAKAR, Senegal
WATU nane wamekufa na wengine 49 wameumia baada ya ukuta wa uwanja wa soka kuwaangukia watu  nchini Senegal.

Janga hilo lilitokea kwenye Uwanja wa Demba Diop katika mjini mkuu, Dakar, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi kati ya Stade de Mbour na Union Sportive Ouakam.

Mapigano yalianza kati ya mashabiki wa timu pinzani na polisi kuingilia kati kwa kutumia mabomu ya machozi, yaliyosababisha mashabiki kuchanganyikiwa, kukimbia ovyo kukanyagana, na baadae ukuta kuanguka.

Baadhi ya mashabiki walikuwa wakirusha vitu yakiwemo mawe kwa wenzao na kusababisha vurugu kubwa.

Picha zilizosambazwa katika mitandao ya kijamii zilionesha watu wakigombea kupanda ukuta,  huku wingu la gesi ya machozi likitanda eneo hilo la uwanja.

Shirika la Habari la hapa (APS) liliripoti kuwa, magari ya kubeba wagonjwa na yale ya zima moto yalikuwepo katika eneo hilo la tukio.

Wakati matokeo yakiwa 1-1 baada ya kumalizika kwa dakika 90, Mbour walifunga katika kipindi cha kwanza cha nyongeza na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, na vurugu kutimka baada ya filimbi ya mwisho.

Cheikh Maba Diop, ambaye rafiki yake alikufa katika tukio hilo na ambaye alisaidia kuondoa watu nje ya uwanja, aliliambia Shirika la Habari la AFP: “Wakati ukuta ulipoanguka…tulijua baadhi ya jamaa zetu watakuwa wamepoteza maisha kwa sababu ukuta ule uliwaangukia watu moja kwa moja.”


Msemaji wa Rais wa nchi Macky Sall alisema kampeni za Urais zilizokuwa zifanyike leo Jumapili ziliahirishwa ikiwa ni sehemu ya maombolezo hayo.

No comments:

Post a Comment