Monday 31 July 2017

Kumekucha maandalizi Bagamoyo Marathon 2017

Na Mwandishi Wetu
MAANDALIZI ya mbio za nne za Kihistoria za Bagamoyo zitakazofanyika Jumapili, Agosti 6, mjini humo, yamepamba moto.

Mratibu wa mbio hizo, Dominic Mosha alisema jana kuwa maandalizi yanakwenda vizuri na wanatarajia zaidi ya wanariadha 500 kushiriki mbio hizo mwaka huu.

Alisema mbali na mbio kuu za kilometa 21, pia kutakuwa na mbio za kilometa 10 na zile za kujifurahisha za kilometa tano ambazo hazina zawadi lakini kila mshiriki atapata fulana.

Alisema washindi watatu wa kwanza wa mbio za kilometa 10 kila mmoja ataondoka na medali.

Alisema mbio za mwaka huu zitakuwa na msisimko wa aina yake na zitaandaliwa kwa ubora zaidi, kwani kila mwaka wanapata uzoefu zaidi wa kuandaa kitu bora.

Mosha aliwataka washiriki kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo, ambazo ni maalum kwa ajili ya kutangaza mji wa kihistoria wa Bagamoyo.

Alisema kuanzia leo wanatarajia kuweka vituo vya usajili wa shiriki ili kuwawezesha wengine ambao hawajaweza kujisajili katika mtandao kufanya hivyo.
Mbio hizo hufanyika kila mwaka na kuandaliwa na 4Bell, ambapo lengo ni kuibua na kuendeleza vipaji pamoja na utalii mjini Bagamoyo na vitongoji vyake.

Mwaka jana mbio hizo zilifanyika Julai 24 na kushirikisha washiriki kibao kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.


No comments:

Post a Comment