Sunday 30 July 2017

Waziri Mwakyembe kuiaga timu ya riadha inayokwenda London kwa mashindano ya dunia

Mwanariadha Alphonce Simbu akimaliza mbio za Mumbai Marathon.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kesho atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuiaga timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya 166 ya Dunia yatakayofanyika jijini London, Uingereza  kuanzia Agosti 4 hadi 13.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mawasiliano wa DStv, Johson Mshana, Mwakyembe atakabidhi bendera hiyo kwa timu hiyo katika hafla itakayofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Timu hiyo ambayo iko chini ya Kocha Mkuu, Zakaria Barie ina wachezaji nane, ambao ni Alphonce Simbu, Stephano Huche na Said Makula ambao watakimbia marathon wakati Gabrie Geay na Emmanuel Giniki watashiriki mbio za meta 5,000 huku Sara Ramadhani na Magdalena Shauri watashiriki marathon kwa upande wa wanawake na Failuna Abdi atashiriki meta 10,000.
Wengine watakaokuweo katika timu hiyo itakayoondoka nchini keshokutwa Jumanne ni pamoja na Francis John, ambaye ni kocha msaidizi wa timu hiyo.

Barie akizungumza kutoka Arusha jana  kwa njia ya simu alisema kuwa timu hiyo imejiandaa vizuri na iko tayari kupambana kwa ajili ya kupata medali kutoka katika mashindano hayo, ambayo kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata medali mwaka 2005 kutoka kwa Christopher Isegwe aliyepata medali ya fedha katika maratoni mashindano hayo yalipofanyikia Helsinki, Finland.

Kocha huyo alisema kuwa timu yake haina majeruhi wowote na inaondoka ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa kabisa ya riadha duniani.
Alphonce Simbu (kushoto) akiwaongoza wenzake katika mazoezi ya timu ya taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya dunia baadae mwezi huu.
Naye Simbu alisema kuwa wamejipanga kurudi na medali licha ya ugumu uliopo mbele yao,  kwani wanajua ushindani mkali uliopo mbele yao.

Hafla hiyo imedhaminiwa na DStv, na tayari Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday aliondoka jana kwenda London kuhudhuria vikao vitakavyofanyika mapema kabla ya kuanza kwa mashindano hayo akimwakilisha rais wake, Anthony Mtaka.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe (mwenye kifimbo) atakuwa mgeni rasmi katika kuagwa kwa timu ya taifa ya riadha kesho. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda.
 Aidha, mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kwani wanariadha bora wawili duniani, Usain Bolt wa Jamaica na Mo Farah wa Uingereza watastaafu rasmi mbio baada ya kushirikiria ubingwa wa dunia kwa muda mrefu,
Hizo zitakuwa mbio za mwisho kwa Bolt katika mashindano ya dunia na Farah naye hatakimbia tena mbio za meta 5,000 na 10,000 au mbio za uwanjani na badala yake atageukia marathon, ambazo ni mbio za kilometa 42.

No comments:

Post a Comment