Thursday 20 July 2017

Mwanamuziki mkongwe Roy Mukuna afariki dunia

Na Mwandishi Wetu
MWANAMUZIKI mkongwe nchini Roy Mukuna (kulia) amefariki dunia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, imeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kiongozi wa kundi la Wazee Sugu, King Kikii, Mukuna alifariki dunia baada ya kulazwa kwa muda katika hospitali hiyo kutokana na maradhi ya figo na ini.

Mukuna mwenye umri wa miaka 47 wakati wa uhai wake alipitia katika makundi mbalimbali akipiga zana tofauti tofauti kabla ya kupuliza saxophone hadi umauti unamkuta.

Msanii huyo hadi anafariki alikuwa kiongozi wa kundi la muziki wa dansi la Bana Kamanyola ambalo linapiga muziki wake katika klabu ya Mwanza ya Villa Park iliyopo karibu kabisa na Uwanja wa CCM Kirumba.

King Kikii amesema kuwa kifo cha Mukuna ni pigo kubwa kwani kimeacha pengo kubwa katika tasnia ya muziki hapa nchini kutokana na umahiri wake.

Naye rafiki wa karibu wa Mukuna, Parash Mukumbule amesema leo kuwa marehemu wakati wa uhai wake alipigia bendi mbalimbali ikiwemo Maquiz, ambako alitunga kibao cha Scola, Super Tanza, Sendema na Deka Musica.

Anasema kuwa marehemu ameacha mke na watoto watano na mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake karibu na mzunguko wa Kigogo jijini Dar es Salaam.


Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina.

No comments:

Post a Comment