Monday 24 July 2017

Rais Magufuli aagiza ujenzi wa jengo la abiria 500 Kiwanja cha Ndege Tabora uanze mara moja

Rais John Pombe Magufuli akipewa maelezo na Mhandisi wa ukarabati, ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora, Neema Joseph wakati wa uzindizi wa mradi huo mkoani humo. Kushoto kwa rais ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Mwandishi Wetu, Tabora
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk  John Pombe Magufuli ameagiza ujenzi wa mradi wa jengo  la abiria 500 kwenye Kiwanja cha Ndege cha Tabora uanze mara moja.

Rais ametoa kauli hiyo mara baada ya kufungua ujenzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora, ambapo alisema sasa abiria wataongezeka kutokana na kukamilika kwa ujenzi huo, hivyo italazimu jengo kubwa lenye kuchukua abiria 500 kwani la sasa lenye uwezo wa kuchukua abiria 50 halitatosha.
“Ninaimani kubwa kwa ujenzi huu lazima idadi ya abiria itaongezeka zaidi, hivyo kwa hili jengo dogo halitatosheleza abiria watakaoongezeka hivyo, namuagiza Waziri (Makame Mbarawa) kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo hilo kubwa, ,” alisisitiza Rais Magufuli.

Amesema kutokana na ukarabati na upanuzi huo sasa kiwanja hicho kitaruhusu kutua kwa ndege kubwa zaidi za ndani na nje ya nchi, na kufanya wakazi wa mkoa wa Tabora kutumia uisafiri wa ndani kwa kwenda Dar es Salaam, Burundi, Kenya, Rwanda na maeneo mengine.
Amesema anarajia ujenzi huo utakamilika mapema zaidi na atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jengo hilo, ambapo aliwapongeza Wizara pamoja na wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Rais amesema serikali yake inataka maendeleo ya kuwa na viwanja vya ndege vya uhakika, barabara na maji na sio siasa, ambazo hazina tija kwa maisha ya wananchi sasa na baadae.
 “Mimi ni Rais wa Watanzania wote na sio wa CCM pekee na ndio maana ninachochea maendeleo tena ya haraka ambayo yatafanikisha wananchi kuwa na maisha mazuri ikiwa ni pamoja na kuitumia miundombinu katika biashara na maisha yao ya kila siku,” amesema Rais.

Katika hatua nyingine, Rais ametaka barabara ya kutua na kuruka kwa ndege irefushwe zaidi ili kuruhusu ndege kubwa kutua kwa wingi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu mbalimbali ya Kiwanja cha ndege cha Tabora.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amesema sambamba na maboresho hayo ya miundombinu katika kiwanja cha ndege cha Tabora, sasa ujenzi wa jengo jipya la abiria unatarajia kuanza mara moja kwa ufadhili wa fedha za mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji ya Uaya (European Investment Bank-EIB), na litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka.

Pia Mbarawa amesema mradi huu wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora umegharamiwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.

Mbarawa amesema mradi huu umejumuisha barabara za kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio, maegesho ya ndege, taa na mitambo ya kiusalama ya kuongoza ndege wakati wowote na kituo cha umeme.
“Kiwanja sasa kimeongezewa uwezo wa kutoa huduma kwa saa 24, na vilevile maboresho yanayofanyika katika viwanja viwanja vya ndege yanalengo la kuvutia ujaji wa mashirika mengi zaidi ya ndege pamoa na kuongeza uwezo wa kuhudumia ndege nyingi zaidi, na sasa serikali inadhamiria ya kununua ndege nne na jum;a itafanya idadi ya ndege sita,” amesema  Mbarawa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kiwanja cha Ndege Tanzania (TAA), Salim Msangi amesema ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja cha ndege cha Tabora umefanyika kwa awamu tatu, ambapo ni kujenga barabara ya kwanza ya kuruka na kutua kwa ndege kwa kiwango cha lami kwa urefu wa mita 1900 na upana wa mita 30.

Msangi amesema awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa barabara ya pili ya kuruka na kutua kwa ndege kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 1260 na upana wa mita 23; maegesho ya ndege yenye uwezo wa kuegesha ndege tatu zenye ukubwa wa ATR 72 au Bombardier dash 8 Q400 kwa wakati mmoja; kujenga kiungio yenye urefu wa mita 250; usimikaji wa taa na mitambo ya kuongezea ndege wakati wa kutua na kuruka.

“Hii awamu ya pili ilihusisha vitu vingi ikiwepo pia ujenzi wa kituo cha kufua umeme na usimikaji wa jenereta lenye kVA 500; ujenzi wa uzio wa usalama wa urefuwa kilometa 2.6 na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua,” amesema Msangi.

Amesema awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka; ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani na eneo la maegesho ya magari, ambapo kwa ujumla utafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na utagharimu sh  za Kitanzania Bilioni 27.

No comments:

Post a Comment