Tuesday 25 July 2017

Timu ya Madola iliyotwaa medali kurudi Alhamisi

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya sita ya Jumuiya ya Madola kwa vijana na kutwaa medali ya shaba inatarajia kutua nchini keshokutwa Alhamisi kutoka Nassau, Bahamas.

Mwanariadha Francis Damas alitwaa medali hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu katika mchezo wa mbio za meta 3,000 kwa kutumia dakika 8.37.51 nyuma ya Mkenya na Mcanada walimaliza katika nafasi ya kwanza na pili.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema jana kuwa, timu hiyo yenye wanariadha wawili na waogeleaji wawili, itatua nchini majira ya mchana kwa ndege ya Emerates.

Kwa medali hiyo, Damas anakuwa Mtanzania wa pili kutwaa medali kutoka katika michezo hiyo baada ya Mary Naali aliyetwaa medali kama hiyo katika michezo ya mwaka 2008 iliyofanyika Pune, India kwa upande wa wanawake.

Tangu wakati huo Tanzania haijawahi kutwaa medali kutoka katika michezo iliyofuata ya mwaka 2011 huko Iron Man, Marekani, ambako hatukushiriki na ile ya Samoa (2015), tulitoka mikono mitupu.

Mbali na kutwaa medali, mwanariadha mwingine wa Tanzania Reginal Mpigachai ambaye alitinga fainali ya mbio za meta 800 licha ya kumaliza katika nafasi ya nane, aliboresha tena muda wake binafsi.
Mpigachai awali katika hatua ya nusu fainali alimaliza watano kwa kutumia dakika 2.11.65 na kuboresha muda waka bora wa awali wa dakika 2.13.51 aliouweka katika mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salam.

Katika fainali za meta 800, Mpigachai alimaliza katika nafasi ya nane, huku akitumia dakika 2.10.57 na kuboresha zaidi muda wake bora.
Sio tu kwa vijana hata kwa wakubwa, Tanzania kwa muda mrefu haijapata kutwaa medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, ambapo kwa mara ya mwisho kwa wakubwa ilitwaa mwaka 2006 kutoka kwa Samson Ramadhani na Fabian Joseph waliotwaa medali za dhahabu na fedha katika marathon.

No comments:

Post a Comment