Sunday 5 August 2018

Rais Maduro wa Venezuela Anusurika Kuuawa


CARACAS, Venezuela
RAIS wa Venezuela, Nicolás Maduro anasema kuwa amenusurika kuuawa katika jaribio la mauaji yaliyohusisha ndege ndogo zisizo na rubani, ambazo zilibeba vilipuzi.

Maduro wakati huo alikuwa akihutubia katika hafla ya kijeshi jijini hapa wakati jaribio hilo la kumshambulia lilipotokea.

Rais Maduro na mkewe, Cilia Flores, ndio walilengwa katika shambulio hilo wakati akihutubia mamia ya askari jijini hapa.
 
Wawili hao, ghafla waliangalia juu kutoka stejini huku mamia ya askari wakikimbia kunusuru maisha yao baada ya kusikia sauti ya mlipuko na kutokea moshi mkubwa angani.

Picha zilionesha baadhi ya askari waliokuwepo katika eneo hilo wakivujwa damu.

“Matangazo mubashara `Live’ ya hotuba yake yanaonesha rais ghafla aliangalia juu, huku mamia ya askari wakikimbia kutoka katika mistari waliyokuwa wamejipanga wakisikiliza hutuba hiyo, “kilisema chanzo kimoja cha habari.

Bwana Maduro ameilaumu Colombia kwa shambulio hilo, dai ambalo limekanushwa na Bogota na kusema halina msingi wowote.

Askari saba waliumia, na watu kadhaa baadae walikamatwa, mamlaka ya Venezuela ilisema.

NINI KILITOKEA?
Tukio la shambulizi hilo, lilitokea wakati Bwana Maduro alikuwa akihutubia katika sherehe ya Kumbukumbu ya Jeshi kutimiza miaka 81.
 
Ndege mbili zisizo na rubani zikiwa na vilipuzi ziliruka jirani na jukwaa alikokuwa rais huyo akihutubia, alisema Waziri wa Mawasiliano Jorge Rodriguez.

Rais Maduro baadae akilihutubia taifa alisema: "Kuna kitu kilichokuwa kikiruka angani, kililipuka karibu yangu, mlipuko mkubwa. Dakika chache baadae kulikuwa na mlipuko wa pili.”
 
Picha katika mitandao ya kijamii zilionesha walinzi wakimlinda Bwana Maduro, huku wakiwa na ngao zisizopitisha risasi `bulletproof shields’ baada ya tukio hilo la uvamizi.

Rais huyo aliwatuhumu majirani zake Colombia na wapinzani wenye msimamo mkali wanaoungwa mkono na Marekani, kuwa ndio walitaka kumuua.

Aliongeza kuwa hana ‘wasiwasi’ Rais wa Colombia Juan Manuel Santos “alihusika katika jaribio hilo”.

Kiongozi huyo wa Venezuela, ambaye awali alikuwa akiituhumu Marekani kumpinga, hakuwa na ushahidi wowote kudhihirisha madai yake.

Hatahivyo, serikali ya Colombia imekanusha kujihusisha kokote na tukio hilo, ikisema kuwa madai hayo ya Bwana Maduro hayana msingi wowote.

No comments:

Post a Comment