Tuesday 7 August 2018

Kipa Chelsea Akaribia Kutua Real Madrid


LONDON, England
KIPA wa Chelsea, Thibaut Courtois, ambaye amekuwa akihusishwa na kutaka kuhamia Real Madrid, hajaripoti katika mazoezi ya timu hiyo ya Ligi Kuu ya England juzi.

Inaelezwa kuwa, the Blues hadi sasa hawajui lini kipa huyo wakimataifa wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 26, atarudi kundini katika kikosi hicho cha Chelsea.

Courtois amekuwa mchezaji wa Blues tangu mwaka 2011, wakati aliposajiliwa kutoka klabu ya Ubelgiji ya Genk na alichukuliwa kwa mkopo na Atletico Madrid.

Winga wa Chelsea, Eden Hazard naye pia amekuwa akihusishwa na Real, lakini Jumatatu hakuhudhuria mazoezi na klabu hiyo.

Courtois alitajwa kuwa kipa bora katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Urusi mwaka huu, ambako Ubelgiji iliifunga England katika mchezo wa kusaka mshindi watatu.

Ameichezea Chelsea mechi 154, akicheza mara 58 bila kufungwa.

Akizungumza juzi, kocha mpya wa Blues Maurizio Sarri alisema hana uhakika kama Courtois ataendelea kuwepo katika klabu hiyo.

Alisema: "Kwa sasa Courtois ni kipa wa Chelsea. Sijui huko mbele. Itategemea na klabu, hasa itamtegemea yeye mwenyewe ana msimamo gani na anataka nini, lakini ninategemea Courtois ataendelea kuwa kipa wetu.”

Taarifa zingine zinasema kuwa, Chelsea wako tayari kutoa kiasi cha pauni milioni 89 ili kumnasa kipa wa Atletico Madrid, Jan Oblak kama mbadala wa Thibaut Courtois kama kipa huyo ataondoka kwenda Real Madrid.

No comments:

Post a Comment