Monday 20 August 2018

Bonanza la Michezo Uchukuzi Kufanyika Jumamosi


Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la Kwanza la Michezo la Uchukuzi linatarajia kufanyika Jumamosi Agosti 25 kwenye viwanja vilivyopo katika jengo la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)  Banana Jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Katibu Mkuu wa Uchukuzi Sports Club (USC), Mbura Tenga alisema juzi kuwa, kikao cha viongozi wa Uchukuzi, ambacho kilifanyika Agosti 13 mwaka huu, kiliamua tamasha hilo la michezo kwa ajili ya watumishi wa Uchukuzi, lifanyike siku hiyo.

Kikao hicho kiliamua kwa kauri moja kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk Leonard Chamuriho ndiye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo la michezo litakaloanza saa 12:00 asubuhi hadi saa 4:00 Asubuhi.
Tenga alisema kuwa tamasha hilo la kwanza pia litatumika kuzindua mazoezi kwa kila taasisi kwenye maeneo ya kazi pamoja na mazoezi ya kujiandaa na Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (Shimiwi).

Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ndilo imeteuliwa kuwa mratibu wa kwanza wa tamasha hilo la kwanza la michezo kwa Sekta ya Uchukuzi.

Katibu huyo alisema kuwa katika kuongeza hamsha hamsha katika tamasha hilo, uongozi wa USC umewaalika waandamizi wa Wizara, Wakurugenzi Wakuu, Wakurugenzi wa Idara zinazojitegemea, Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali na Watumishi waliopo chini ya sekta ya Uchukuzi.
Alisema ni matumaini yao kuwa ushiriki wa wahusika wote watashiriki na kuamsha chachu ya mazoezi na hatimaye kuimarisha afya za watumishi wa Uchukuzi.

No comments:

Post a Comment