Wednesday 8 August 2018

Kiwanja cha Ndege cha Simiyu Ni cha Kipekee




1.    Wanafunzi kutoka shule ya Sekondari ya Wahaha ya Bariadi wakimsikiliza Afisa Usalama Mwandamizi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Bakari Mwalwisi (kulia) akitoa elimu ya namna ya kusafiri na mizigo kwenye ndege, leo walipotembelea banda la maonesho ya Kilimo kwenye Uwanja wa Nyakabindi, mkoani Simiyu.
Na Mwandishi Wetu, Simiyu

KIWANJA kipya cha ndege cha mkoa wa Simiyu kinachotarajiwa kuanza kujengwa baadaye mwaka huu, kitakuwa cha kipekee kwa kuwa ndio cha kwanza cha serikali kuwa karibu na mbuga ya wanyama, imeelezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema hivi karibuni alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), yanayofanyika kwenye Uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu, kuwa kiwanja hicho ndicho kitakuwa mpakani mwa mbuga ya wanyama ya Serengeti.

1.    Ofisa Biashara na Masoko Mwandamizi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Herieth Nyalusi (kulia), akitoa maelezo mbalimbali kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu, walipotembelea banda la maonesho ya Kilimo la TAA leo kwenye Uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu.

“Kuna kitu nadhani tulikosea kwa kuweka viwanja vingi vya ndege mbali sana na mbuga na hifadhi zetu za wanyama, na inasababisha tukose mapato zaidi, mfano unatoka Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro hadi Serengeti ni umbali wa Km 400, au Mwanza hadi Serengeti ni Km 200 na kutoka Mara ni Km. 150, kote huko ni mbali, lakini hiki cha Simiyu kipo karibu Zaidi,” alisema Mtaka.

Hata hivyo, Mhe. Mtaka alisema kutokana na kiwanja hicho kuwa cha kwanza, karibu na mbuga hivyo, wanaipa mbuga hiyo heshima kwa kukiita Kiwanja cha Ndege cha Serengeti, ambapo amewataka TAA kuhakikisha wanafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili waweza kuanza ujenzi huo haraka.

1.        Bi. Cecilia Mpanju wa Shirika la Mawasiliano nchini (TTCL) leo akipata maelezo ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII), kutoka kwa Afisa Mipango na Takwimu, Bw. Edward Kimaro, wakati alipotembelea banda la maonesho ya Kilimo la Mamlaka kwenye Uwanja wa Nyakabindi, mkoani Simiyu.

Lakini ameitaka TAA ishirikiane na wadau wengine wakiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili kuhakikisha kinajengwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa, ambacho kitaruhusu ndege kubwa kutoka nchi za nje na kutua moja kwa moja Simiyu na watalii waweze kufika kwa urahisi kwenye mbuga ya Serengeti, ambapo mbali na mbuga pia wanaweza kutembelea Ufukwe wa Busega uliopo wilaya ya Busega.

“Serikali ya mkoa ipo tayari kusaidiana na TAA na imeshaanza mazungumzo na wananchi waliopo maeneo ya Igegu ambapo ndipo kiwanja kitakapojengwa, ili waridhie kupisha ujenzi huo, ambao utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi,” alisisitiza Mhe. Mtaka.

1.        Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dr. Mbura Omar (kushoto), akimsikiliza Ofisa Tehama Mwandamizi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw.Geofrey Youze leo kwenye banda la maonesho ya Kilimo yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu kwenye uwanja wa Nyakabindi.


Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alisema kiwanja hicho kitarahisha usafiri wa anga kwa wakazi na wageni watakaokuwa wakitoka maeneo mbalimbali kwa shughuli za kibiashara na kitalii, ambapo pia kitapunguza gharama kubwa ya nauli za usafiri wa ndege ambao utapungua kwa ndege nyingi kutua Simiyu.

Bw. Mayongela amewataka wananchi wa Simiyu kutumia fursa ya kujengwa kwa Kiwanja hicho cha ndege kwa kujenga miundombinu mbalimbali zikiwemo nyumba za kulala wageni, migahawa ya kisasa na usafiri wa magari.

1.     Wakuu wa Wilaya za Itilima na Bariadi, Mhe Benson Kilangi (wa kwanza kushoto) na Mhe. Festo Kiswaga (katikati) wakipata maelezo ya ujenzi wa Kiwanja kipya cha ndege kutoka kwa Mwanasheria Mwandamizi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Janet Mugini walipotembelea banda la maonesho ya Kilimo la Mamlaka kwenye uwanja wa Nyakabindi mkoani Simiyu.

“Huu mkoa wa Simiyu unawatu wanaofanya shughuli mbalimbali zikiwemo za biashara ya mazao ya chakula na biashara na madini, hivyo kupatikana kwa kiwanja hiki kutawaongezea fursa za shughuli zao kupanuka zaidi, ikiwemo shughuli ya kuhudumia watalii wa ndani na nje ya nchi watakaokuja kutembelea mbuga kubwa ya wanyama ya Serengeti,” alisema Bw. Mayongela.

Hata hivyo Bw. Mayongela alisema kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) watahakikisha zoezi la ulipwaji fidia kwa wananchi waliopo karibu na eneo kitakapojengwa kiwanja hicho linafanyika kwa haraka ili ujenzi uweze kuanza kwa kutokuwa na kipingamizi chochote.

 “Ninawasii ndugu zangu wa Igegu kuleta madai ya fidia zinazolingana na makazi yao na msileta madai makubwa ya kudanganya kwani yatasababisha serikali ishindwe kuwalipa na kufanya Kiwanja hiki kisijengwe kwa wakati uliopangwa,” amesema Bw. Mayongela.

No comments:

Post a Comment