Saturday, 19 May 2018

Wanausalama Viwanja vya Ndege WaimarikaKaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (katikati waliokaa), akiwa kwenye picha ya pamoja na wakufunzi na washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa kwa ndege, mara baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo jana katika Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo Jengo la Kwanza la abiria la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. (Picha zote na  Bestina Magutu wa TCAA).Na Bahati Mollel,TAA
WANAUSALAMA wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini, wameiva na kuimarika katika usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa kwa njia ya ndege baada ya jana kufuzu mafunzo yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), iliyofanyika kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Wakati akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Vedastus Fabian kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, amewataka wahitimu hao kutumia vyema ujuzi walioupata kwa kufanyakazi kwa ufanisi na kuboresha kazi hiyo, ili kuepuka kupitisha mizigo hatarishi kwa usalama wa usafiri wa anga.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (aliyesimama) akiwahutubia wahitimu wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo (hawaonekani pichani) wakati akifunga mafunzo hayo jana kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).


“Tunavyojua mfumo wa usafiri wa anga duniani ni moja kwa hiyo tunavyoonesha usalama katika viwanja vyetu vya ndege hapa Tanzania kunajenga imani kubwa kwa mashirika ya ndege na wadau wote wanaofanya shughuli nakutumia viwanja vyetu vya ndege, hivyo tutaongeza wingi wa mizigo,” amesema Fabian.

Hata hivyo, alitoa pongezi kwa wahitimu wote 19 kwa kuweza kufaulu vyema mafunzo hayo, ambapo sasa watakuwa na weledi na ufanisi bora katika kazi hiyo.

Amesema TAA inategemea mafunzo hayo yataleta manufaa na sio kuonesha vyeti ukutani kuwa wamehitimu bali ni kuonesha ujuzi walioupata kutasaidia kutambua mizigo na vifurushi vyenye matatizo ya kutishia usalama wa anga na kuongeza uhakika wa safari za anga.

Mkufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), Bw. Sunday Mweemba wa Zambia akielezea namna walivyotoa mafunzo kwa wahitimu wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo akishirikiana na mkufunzi mwenzake Bw. Ernest Bongane wa Afrika ya Kusini, wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyomalizika jana kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).
Fabian pia amesema wanategemea washiriki kufikisha na kusambaza ujuzi huo kwa wanausalama wengine, ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo adimu, ili nao waboresha kazi zao.

Hali kadhalika amewataka washiriki kujiendeleza zaidi kwa kupata mafunzo  mbalimbali ya masuala ya usalama katika usafiri wa anga, kwa kuwa wahalifu wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali kila wakati.

Naye Kaimu Meneja wa Usalama wa TAA, Julius Misollow amesema washiriki wote wameiva kwa kutambua na kubaini mizigo na vifurushi vyenye utata na vyenye kutishia usalama wa usafiri wa anga nchini.

Missolow amesema wahitimu hao wataendelea na mafunzo ya ukufunzi, ambapo wakihitimu wataisaidia mamlaka kwa kutengeneza wataalam zaidi wa masuala ya usalama, ambao watapunguza gharama za kutumia wakufunzi kutoka nje ya nchi.

Naye mmoja wa wakufunzi hao Sunday Mweemba kutoka Zambia amesema washiriki wote wamepata mafunzo ya msingi kwa upana, ambapo yataisaidia nchi kufanya vizuri katika usalama wa  usafiri wa anga.

Washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo wakimsikiliza mgeni rasmi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (hayupo pichani) aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu, wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika jana kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Mweemba amesema mafunzo haya yamekuwa yakitolewa nje ya nchi, lakini ameishukuru menejimenti ya TAA kwa kujitoa kwa hali na mali na kufanikisha kuwaleta wakufunzi hapa nchini ili wanausalama wengi zaidi waweze kushiriki, endapo yangeendeshwa nje ya nchi wangeshiriki wawili au mmoja.

Kwa upande wa wahitimu, Bw. Wenceslaus Sango ameishukuru menejimenti ya TAA kwa kufanikisha mafunzo hayo, wakufunzi na mratibu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Bw. Burhan Majaliwa, ambapo wameahidi kuyatumia vyema kwa faida ya taifa.

Washiriki walioshiriki na viwanja wanavyotoka kwenye mabano ni pamoja na Mohamed Makau (TAA Makao Makuu), Zalia Msangi na Stephen Magambo (Arusha); Philbert Lyimo, Ahmed Zomboko, Thawabu Njeni, Rehema Mlanzi, Nuhu Kisweswe, Martha Kilunga, 

Levina Valasa, Josephine Kahimba, Anna Myovela, Fatma Shomari na Stephen Ntambi (JNIA);.

Wengine ni   Felister Lutonja (Shinyanga) Mathias Gombo, Lilian Malero na Wenceslaus Sango (Mwanza)  na Bebedict Ole Laput (Songwe).

No comments:

Post a Comment