Tuesday 22 May 2018

TAA Yaandaa Mikakati Kudhibiti Viashiria Hatarishi

Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Ndani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Irene Sikumbili (aliyenyoosha mkono kulia), akitoa ufafanuzi kwa washiriki wa mafunzo ya Viashiria hatarishi (Risk Management) yanayohusisha Watumishi wa Mamlaka hiyo, yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Veta jijini Dar es Salaam.
 
Mwandishi Maalum
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeanza mikakati ya kujiwekea mfumo wa viashiria hatarishi (Risk Management) kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake, ambayo yameanza jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) uliopo Kipawa jijini Dar es Salaam.
 Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Bw. Dickson Austin (aliyesimama) akifundisha washiriki wa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), jana kwenye ukumbi wa VETA Kipawa jijini Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, ambayo yanashirikisha washiriki kutoka Idara mbalimbali, Bw. Lawrence Thobias ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala,  amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatatumika kama sehemu ya kazi, hivyo washiriki wote wazingatie na kujifunza kwa bidii.

“Ninajua wote waliopo kazini wanauwezo na nyie mmechaguliwa wachache na hamuwezi kuja wote katika mafunzo haya, ila ninachowaomba mjifunze kwa bidii na mshirikishane yale mnayoyafahamu, kwani wote hapa ni wazoefu ili kuleta ufanisi bora na mzuri katika Taasisi yetu,” amesema Bw. Thobias.
  Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama) akifungua mafunzo ya siku tano ya kutambua viashiria hatarishi (Risk Management) yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Veta Kipawa jijini Dar es Salaam.
Bw. Thobias amesema kuwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo,  TAA itatengeneza nyaraka za viashiria hatarishi kwa kutumia wataalamu watakaochaguliwa miongoni mwa washiriki, ambazo zikikubalika kwa viwango vinavyotakiwa, basi itatakiwa kusimamiwa na kuendeshwa vyema na Mamlaka.

Naye Naibu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (Usimamizi wa Viashiria Hatarishi, Mfumo na Udhibiti wa Ndani), kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Bw. Emmanuel Subbi kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu, amesema wameamua kutoa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) kwa Taasisi za Serikali ili waweze kuishauri Serikali namna ya kuvizuia na kuvidhibiti kabla ya kutokea.
      Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi anayeshughulika na Usimamizi wa Viatarishi hatarishi, Mifumo na Udhibiti wa Ndani, Bw. Emmanuel Subbi kutoak ofisi ya Mkaguizi Mkuu wa Hesabu, akionesha Mwongozo wa serikali wa mwaka 2012 kwa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Viashiria hatarishi (Risk Management) wanaotoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Bw. Subbi amesema kila Taasisi inatakiwa kuwa na mwongozo wa viashiria hatarishi wa mwaka 2013 na pia Waraka wa Hazina namba 12 wa mwaka 2013, ambapo zote zinaonesha namna na jinsi ya kuzuia viashiria hatarishi.

“Mfumo huu una faida kubwa kwa Taasisi za Umma kwani unasaidia kuaminika na hata kupata mikopo kutoka katika Taasisi mbalimbali Duniani, pia mfumo huu utakupa nafasi nzuri ya kufanya maamuzi kwa upana ikiwa unaangalia na mfumo wako wa kazi,” amesema Bw. Subbi.
 Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias (wa kwanza kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki na wakufunzi wa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) yanayofanyika kwenye ukumbi wa Veta-Kipawa, jijini Dar es Salaam. (Picha zote Bahati Mollel wa TAA)
Pia Bw. Subbi amesema mfumo huu utasaidia kuepuka matatizo katika ununuzi, sheria, viwango na udhibiti, ambapo miaka ijayo itapunguza kupatikana kwa hati chafu kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), ambapo mfumo ukizingatiwa hakutakuwa na matatizo hayo kwani watagundua viashiria hatarishi kabla havijatokea na kuleta madhara.


No comments:

Post a Comment