Tuesday 1 May 2018

Nyota ya Mohamed Salah Yaendelea Kung'ara


LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa Liverpool Mohamed Salah (pichani) ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari za Soka.

Kiungo wa Manchester City Kevin de Bruyne ameshika nafasi ya pili huku mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane akiibuka watatu.

Salah, mwenye umri wa miaka 25, amefunga mabao 31 katika mechi 34 za ligi alizoichezea timu hiyo msimu huu.

Nyota huyo wa Misri, ni mwanasoka wa kwanza wa Afrika kupewa tuzo hiyo, ambaye pia alitwaa tuzo kutoka kwa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa mwezi uliopita.

Mshambuliaji wa Chelsea na England Fran Kirby ameshinda tuzo ya uchezaji bora wa mwaka kwa wanawake (FWA).

Salah amefunga mabao 43 katika mashindano yote baada ya kusajiliwa na Liverpool kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 34 akitokea Roma ya Italia.

Mchezaji huyo wazamani wa Chelsea na Basel alifunga mara mbili katika mchezo wa kwanza wakati Liverpool ikiibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Roma katika mchezo wa nusu wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwenye Uwanja wa Anfield wiki iliyopita.

Kikosi cha kocha Jurgen Klopp tayari kiko Italia kwa mchezo wa Jumatano dhidi ya Roma utakaofanyika kwenye Uwanja wa Stadio Olimpico kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano.

MBIO ZA WACHEZAJI WAWILI

Salah na mchezaji mwenye umri wa miaka 26 Mbelgiji De Bruyne alipata zaidi ya asilimia 90 ya kura zilizopigwa na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Soka.

Mwenyekiti wa FWA Patrick Barclay alielezea mpambano wa wawili hao kama ni wa nguvu zaidi tangu mwaka 1968-69", wakati walipopambana kati ya Tony Book wa Manchester City na yule wa Derby, Dave Mackay.

Wachezaji wengine waliopigiwa kura na wanachama wa FWA walikuwa: Sergio Aguero (Man City), Christian Eriksen (Tottenham), Roberto Firmino (Liverpool), Nick Pope (Burnley), David Silva (Manchester City), Raheem Sterling (Man City) na Jan Vertonghen (Tottenham).

No comments:

Post a Comment