Friday 25 May 2018

Yanga Wanusurika Kupapaswa na Ruvu Shooting


Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wazamani wa Soka Tanzania Bara, Yanga jana walinusurika kupapaswa na Ruvu Shooting katika mchezo uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam baada ya kulazimishwa sare ya kufungana 2-2.

Kwa matokeo hayo, Yanga sasa imefikisha pointi 52 ikiendelea kuwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC iliyopo katika nafasi ya pili na Simba inayoongoza na tayari imeshatwaa ubingwa.

Yanga waliandika bao la kwanza katika dakika ya 17 lililofungwa na Matheo Anthony baada ya kuunganisha  kifundi krosi ya Pappy Shishimbi.

Yanga waliutawala mchezo huo katika kipindi cha kwanza na kulishambulia lango la wapinzani wao mara kwa mara, lakini walikosa mabao mengi baada ya kushindwa kutumia nafasi kibao walizopata.

Vijana wa Ruvu Shooting walipambana na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha kupitia kwa penalti iliyowekwa kimiani na Hamis Mcha baada ya beki wa Yanga, Abdallah shaibu kuushika mpira katika eneo la hatari.

Yanga nusura wafunge bao la pili katika dakika ya 33 wakati Kamusoko alipokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lakini liligonga mtambaa panya na mpira kurudi uwanjani na kuokolewa.

Baada ya mashambulizi ya hapa na pale,Yanga walifanikiwa kuandika bao la pili lilifungwa na Maka Edward kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Tshishimbi.

Timu hizo hadi zinakwenda mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kiloanza kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, lakini Ruvu Shooting ndio walikuwa na bahari baada ya kupachika bao la kusawazisha katika dakika ya 49 kwa bao lililowekwa kimiani na Issa Kanduru.

Full Maganga alipoteza nafasi ya wazi kuifungia Rivu Shooting bao la ushindi, lakini akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, alipiga shuti lililokwenda nje ya lango na kuikosesha timu yake bao.

Vikosi vilikuwa; Yanga: Ramadhani Kambwili, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Said Juma, Maka Edward, Pius Buswita, Papy Tshishimbi, Matheo Anthony, Thabani Kamusoko na Emmanuel Martin.

Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, George Aman, Yusuf Nguya, Amissi Kisanga, Rajabu Zahir, Baraka Mtui, Abrahman Mussa, Shaban Msala, Issa Kanduru, Fullu Maganga na Amissi Mcha.

No comments:

Post a Comment