Saturday 27 May 2017

Simba mabingwa wapya Kombe la FA 2017

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SIMBA ya Dar es Salaam leo imekata tiketi kupanda ndege baada ya kutwaa taji la Kombe la FA kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbao FC katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Simba iliandika bao la kwanza katika dakika ya 95 ikiwa ni dakika tano tangu muda wa nyongeza uanze, lililofungwa na Fredricka Blagnon aliyeingia akitokea benchi na kuzua shamra shamra kwa wapenzi wa Simba.

Mbao FA walisawazisha bao hilo kupitia kwa Ndaki Robert katika dakika ya 110 baada ya mabeki wa Simba kufikiri kuwa mfungaji ameotea.

Simba walipata penalti katika dakika ya 121 baada ya mchezaji mmoja wa Mbao FC kuunawa mpira katika eneo la hatari baada ya kutokea piga nikupige na Shizza Kichuya alifunga penalti hiyo.

Kwa taji hilo, Simba sasa itapata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la 
Shirikisho Afrika msimu ujao.

Pius Buswuta wa mbao alikosa bao katika dakika ya nne akiwa ndani ya eneo la hatari, alipiga nje mpira huo.

Simba ilinusurika kufunga mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili wakati Kichuya akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga, alishindwa kufanya hivyo baada ya Yussuf Ndukumana kuokoa.

Juuko nusura afunge lakini alikosa bao baada ya kupiga kichwa na mpira kupanguliwa na kipa wa Mbao FA, Benedict Haule.

Nafasi hii inaiwezesha Simba kupanda ndege baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa takribani miaka minne baada ya kuzikosda nafasi mbili za kwanza na kuwafanya kutoshiriki mashindano ya kimataifa.

Kwa mara ya mwisho Simba ilishiriki mashindano hayo ya kimataifa ni Februari 17, 2013 walipofungwa mabao 4-0 na DC Libolo ya Angola katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Karibu miaka yote minne, Yanga na Azam ndio walikuwa wakipokezana nafasi ya kwanza na pili.
Mbao FC pamoja na kucheza mara ya kwanza Ligi Kuu pamoja na fainali hiyo ya FA, lakini ni timu imara hasa ukizingatia ilizifunga Yanga, Azam FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar katika ligi.

Kwa muda mrefu Simba imekuwa ikiitwa wa matopeni huku Yanga ikiwa ya kimataifa kufuatia timu hiyo kushindwa kufuzu kwa michezo ya kimataifa wakati watani zao walikuwa wakifuzu kila mwaka na kufanikiwa kupanda ndege.

Vikosi vilikuwa Simba: Daniel Agyei, Jamvier Bukungu, Mohamed Hussein, Juuko Murshid, James Katei, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamini Yasin, Laudit Mavugo, Said Ndemla/Fredricka Blagnon na Juma Luizio/Ibrahim Ajibu.

Mbao FC: Benedict Haule, David Mwasa, Salimin Hoza, Asante Kwasi, Boniface Maganga, Yussuf Ndikumana, George Sangija/Dickson Ambundo, Jamal Mwambeleko, Pius Buswita, Habibu Haji/Rajishi Kotecha na Ibrahim Njohole.

No comments:

Post a Comment