Monday 22 May 2017

Wanafunzi wa Filbert Bayi wafanyiwa tafrija nzito kwa kutwaa medali Kanda ya Tano Riadha

Mwenyekiti wa shule za Filbert Bayi, Filbert Bayi akiwa na wanafunzi wa shule hizo baada ya tafrija ya wanafunzi hao baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya umri wa miaka 18 juzi Kibaha mkoani Pwani.
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Filbert Bayi (FBF) imesema kuwa itaendelea kugharamia elimu ya wanariadha watakaofanya vizuri katika michezo na masomo.

Hayo yalisemwa juzi na mwenyekiti wa shule hizo, Bayi wakati wa hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa shule iliyowalioshiriki mashindano ya 12 ya riadha Kanda ya Tano ya Afrika.
Mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 13 na 14 mwaka huu.

Bayi alisema kuwa wataendelea kugharamia ada na mahitaji mengine yote ya wachezaji wenye vipaji ili waendelea kusoma katika shule hiyo iliyopo Mkuza Kibaha mkoani Pwani.

Katika mashindano hayo shule hiyo ilitoa wanariadha watano waliounda timu ya taifa ilishika nafasi ya pili kwa matokeo ya jumla huku ikimaliza ya kwanza kwa upande wa wasichana.

Wanafunzi wa shule hiyo walikuwemo katika timu ya taifa ya Tanzania iliyoshiriki mashindano hayo ni Rose Thesuni alipata medali tatu za dhahabu katkika mbio za meta 400, kuruka juu na zile za kupokezana vijiti za meta 4x400.

Thesuni alipata medali ya fedha katika mchezo wa kupokezana vijiti wa mbio za meta 4x400 huku Bitrina Alexander akipata medali moja ya dhahabu katika mbio za kupokezana vijiti za meta 4x100, medali ya fedha katika meta 4x400 na shaba katika meta 400.
Dorcus Ilanda mwenyewe alipata medali ya fedha katika mbio zakupokezana vijiti za meta 4x400 na medali ya shaba katika meta 800 wakati Regina Mpigachai akipata medali za fedha katika meta 800 na kupokezana vijiti 4x400.

Mwanariadha mwingine wa shule hiyo ni Esther Martin aliyeshiriki mbio za meta 3000 na kumaliza katika nafasi ya nne kwa kutumia dakika 10:23.18.
Mwanafunzi mmoja hugharimu kiasi cha sh milioni  1.6 kwa temu kwa mwanafunzi mmoja, ambapo kwa mwaka kila mwanafunzi anagharamiwa sh milioni 3.2.

Alisema kuwa pamoja na gharama kubwa lakini wataendelea kuwagharamia wanafunzi wenye vipaji ili kuviendeleza vipaji vyao katika mchezo huo.

Naye katibu msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla aliipongeza FBF kwa kuwatunza watoto hao na kuwataka kuendelea kuwagharamia ili kuwajengea msingi wa maisha yao katika michezo na elimu.
Aliwataka wanafunzi hao kutumia muda wao vizuri kwa ajili ya masomo na michezo.

Thesuni aliyepata medali tatu za dhahabu na moja ya fedha alimshukuru Bayi kwa kuwawezesha kugharamiwa elimu na mahitaji mengine na kuahidi kuendelea kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Wanafunzi hao walitwaa jumla ya medali 11, ambapo mbali na kukata keki katika hafla hiyo, pia walipewa zawadi ya fedha taslimu.



No comments:

Post a Comment