Friday 26 May 2017

RT yawashukuru wadau waliofanikisha mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, RT, Wilhelm Gidabuday akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Tullo Chambo.
Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) imewashukuru wadau waliofanikisha kufanyika kwa mafanikio mashindano ya 12 ya riadha ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya vijana yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na Tanzania ilitwaa ushindi wa kwanza kwa upande wa wanawake huku ikishika nafasi ya pili katika ushindi wa jumla.
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday aliwashukuru wadau, kampuni na watu mbalimbali waliofanikisha kufanyika mashindano hayo ya vijana.

Gidabuday alisema kuwa mashindano hayo yalifanikiwa na kufanyika kwake kumewezesha wanariadha 17 wa Tanzania kufuzu kwa mashindano ya dunia yatakayofanyika Nairobi, Kenya Julai 12 hadi 16.
Alisema kama wadau wangeshindwa kujitokeza kusaidia kufanyika kwa mashindano hayo na RT ingeshindwa kuyaandaa, “basi wanariadha wetu wasingeweza kufuzu kwa mashindano hayo ya Dunia.”

Alisema Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) limeipa Tanzania nafasi mbili tu ya kushiriki mashindano hayo, ambao itawagharamia, huku RT ikisaka fedha kwa ajili ya kuwagharamia wanariadha 15 waliobaki.
Aidha, Gidabuday alisema kuwa, RT pia itajitahidi kupeleka wanariadha wengi katika mashindano ya dunia ya wakubwa yatakayofanyika London, Uingereza Agosti.

Pia alisema kwa sasa wanasaka fedha kwa ajili ya kambi za timu hizo mbili, ya vijana na ile ya wakubwa ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri katika mashindano hayo yote.
Wadhamini wa mashindano hayo ni NMB, PPF, Vodacom, Serengeti Marathon na Maji Uhai.

No comments:

Post a Comment