Saturday 27 May 2017

Wanariadha wa Tanzania kulamba mamilioni Marekani katika mbio za Bolder Boulder


Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA wa Tanzania, Josephat Joseph, Ismail Juma na Gabrie Gerald watalamba kitita cha Dola za Marekani 15,000 (sawa na Sh 33,540,000) endapo watashinda mbio za kilometa 10 za Bolder Boulder zitakazofanyika Jumatatu Marekani.

 Waandaaji wa mbio hizo wameandaa kiasi cha dola za Marekani 42,000 (sawa na Sh milioni 94) ikiwa ni zawadi kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa tano kwa wanaume na wanawake. 
Wanariadha wawili wa Tanzania, Joseph na Juma waliondoka nchini juzi kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro kwenda Colorado, Marekani ambako wataungana na Gerald kwa ajili ya mashindano hayo.

 Taarifa za mtandao zilisema kuwa dola 15,000 zinatolewa kwa timu itakayoshinda ambayo itakuwa na wanariadha watatu huku zawadi binafsi kwa mshindi wa kwanza ni dola 3,000. 

Kwa mujibu wa waandaaji, mbio hizo ndizo hutoa zawadi za fedha nyingi kuliko mbio zozote zisizo za marathoni Marekani, ambapo hutoa kiasi cha dola 10,800 katika zawadi binafsi kwa ajili ya washindi 10 wa kwanza. 
Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania, Wilhelm Gidabuday alisema juzi kuwa vijana hao baada ya mbio hizo wanatarajia kutembelea katika Chuo Kikuu cha Adam State kilichopo Almos katika Jimbo la Colorado, Marekani.
Rekodi ya mashindano hayo kwa upande wa wanaume ni muda wa dakika 27:52 wakati ile ya wanawake ni 32:13, ambapo mwanariadha atakayemaliza katika muda mzuri zaidi, atapata bonasi itakayojumuishwa na zawadi za washindi.

No comments:

Post a Comment