Tuesday 16 May 2017

Yanga yatetea ubingwa wake wa Bara

Mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe (kulia) akiwania mpira na kiungo mshambuliaji wa Toto African, Yusuph Mlipili wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. 
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga leo wamefanikiwa kutetea ubingwa wao baada ya kuifunga Toto African ya Mwanza kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 68, ambazo zinaweza kufikia wa Simba, lakini endapo tu Yanga watafungwa katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mbao FC mjini Mwanza Jumamosi.

Pamoja na Simba kuwa na uwezekano wa kuifikia Yanga kwa pointi, lakini ni ndoto kwa timu hiyo kuifunga Mwadui kwa zaidi ya mabao 12.

Yanga ina mabao 57 ya kufunga na kufungwa 13, hivyo ina wastani wa mabao 44 wakati Simba imefunga mabao 48 na imefungwa 16, hivyo ina wastani wa mabao 32 iipitwa na Yanga kwa mabao 12.

Pamoja na katika soka lolote linawezekana, lakini timu kufunga mabao 12 katika mchezo mmoja ni jambo lisilowezekana kwani tangu msimu huu uanze, hakuna timu iliyowahi kufunga zaidi ya mabao hayo.

Katika mechi 29, ambazo Simba tayari imeshacheza, haijawahi kushinda zaidi ya mabao matano, hivyo timu hiyo tayari msimu huu imeshindwa kutwaa taji hilo.

Katika mchezo huo wa jana, Amis Tambwe ndiye aliyeiwezesha Yanga kuondoka na pointi zote tatu na kujihakikishia ubingwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufunga bao katika dakika ya 82 baada ya kupata pasi kutoka kwa Juma Abdul.

Ligi hiyo inatarajia kukamilika Jumamosi kwa mechi za Simba dhidi ya Mwadui ya Shinyanga, Yanga na Mbao FC ya Mwanza, Azam FC na Kagera Sugar, Majimaji na Mbeya City, Stand United dhidi ya Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar na Toto Africans, Prisons na African Lyon na Ndanda FC na JKT Ruvu.

Vikosi vilikuwa:-
Yanga:Beno Kakolanya, Vicent Bossou, Juma Mahadhi/Kaseke, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa na Amis Tambwe.

Toto Africans: Lucajo Lerient, David Kissu, Mohamed Soud, Hamimu Abdu, Ramadhani Malima, Yusuph Mlipili, Carlos Protas, Juvenary Pastory/Waziri Ramadhani, Hussein Kasanga na Waziri Junior.

No comments:

Post a Comment