Sunday 14 May 2017

Tanzania yaonesha nuru mpya katika riadha

Wachezaji,  viongozi na waamuzi wakicheza kwaito baada ya kumalizika kwa mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imeshika nafasi ya kwanza katika mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 kwa upande wa wanawake huku ikishika nafasi ya pili katika ushindi wa jumla katika mashindano hayo yaliyomalifika jana kenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Michezo nchini, Yusuph Singo akimvisha medali mmoja wa wanariadha wa Zanzibar walioshiriki mbio za kuokeana vijiti na kutwaa nafasi ya tatu.

Pia wanariadha 13 wa Tanzania ia wamefuzu kushiriki mashindano ya dunia ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 yatakayofanyika Kenya Julai mwaka huu baada ya kukimbia muda mzuri katika mbio zao.

MATOKEO YA WASICHANA, WAVULANA NA WASHINDI WA JUMLA
Kwa upande wa wanawake, Tanzania ilitwaa medali tano za dhahabu, nne za fedha na tatu za shaba, ikifuatiwa na Kenya akati Sudan ilimaliza ya tatu, Zanzibar ya nne, Eritrea ya tano, Sudan Kusini na Somalia zilifungana katika nafasi ya sita kwa upande huo wa wanawake.
Magwiji wa riadha nchini, Filbert Bayi (kulia) na Juma Ikangaa wakati wa kutoa zawadi kwa washindi wa  mashindano ya riadha ya Kanda ya Tano ya Afrika kwenye Uwanja wa Taifa.
Tanzania ambayo kwa miaka mingi haijafanya vizuri katika mashindano ya riadha kama timu, jana katika mashindano hayo ya vijana kwa ushindi wa jumla, ilijukusanyia medali saba za dhahabu na fedha saba, huku tatu zikiwa za shaba.

Timu ya Tanzania ya mchezo wa mbio za kupokezana vijiti kwa wavulana ndio ilimalizia medali za dhahabu baada ya kushika nafasi ya kwanza huku wasichana wao wakimaliza a pili nyuma ya Wakenya na kupata medali ya fedha.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja akimvisha medali mwanariadha wa Tanzania.

Kama timu ya kupokezana vijiti ya wasichana ya mchezo wa meta 400 x 4 ingepata medali ya dhahabu, basi Tanzania ingekuwa mshindi wa kwanza wa jumla, lakini sasa Kenya ndio ilitwaa ushindi wa jumla wa mashindano ya mwaka huu.

Kenya imeshika nafasi ya kwanza baada ya kutwaa medali nane za dhahabu, nne za fedha ba tatu za shaba wakati Zanzibar ilimaliza ya tatu baada ya kutwaa medali nne za dhahabu, fedha tano na shaba nne.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Sudan ilimaliza ya nne kwa kutwaa medali mbili za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba, wakati Eritrea ilishika nafasi ya tano kwa kuwa na medali tatu za fedha na sita za shaba huku ikiwa haina medali hata moja ya dhahabu.
Sudan Kusini ilimaliza ya sita baada ya kuambulia medali moja tu ya shaba wakati Somalia ilishika mkia baada ya kushindwa kuambulia medali yoyote ile.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya nchi saba, ambazo ni wenyeji Tanzania, Zanzibar, Kenya, Eritrea, Sudan, Sudan Kusini na Somalia wakati nchi ambazo hazikufika ni pamoja na Rwanda, Uganda, Ethiopia na Djibout.
Mashindano hayo ambayo yalifunguliwa juzi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, yalifungwa jana na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Mohamed Kiganja.





No comments:

Post a Comment