Tuesday, 23 May 2017

Manji atangaza kuachia ngazi Yanga

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji ametangaza kuachia ngazi rasmi kuiongoza klabu hiyo, imefahamika.

Kwa mujibu wa Katiba, Yanga sasa itakuwa chini ya uongozi wa Makamu mwenyekiti wake, Clement Sanga hadi pale uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo utakapofanyika.

Akielezea kujiuzulu kwa, Mani alisema kuwa ameamua kukaa pembeni ili kuwapisha wengine nao waiongoza klabu hiyo.

"Nimeamua nipumzike nipishe wengine waongoze, Yanga ni yetu sote nilipoingezewa muda tu kwa demokrasia, lakini haimanishi kuwa Mimi ndio nitakua Mwenyekiti milele, " alisema Manji ambaye hata hivyo si mara yake ya kwanza kutangaza kuachana na klabu hiyo.

Agosti mwaka jana pia alitangaza kujiuzulu  ikiwa ni siku chache tangu alipotangaza kutaka kuikodi timu hiyo kwa muda wa miaka 10, huku asilimia 75 za timu hiyo zikiingia kwake na kutoa asilimia 25 kwa timu hiyo kila mwaka kitu kilichopingwa na wadau wengi wa Soka ikiwemo Serikali.

Hata hivyo, wanachama wa klabu hiyo walimpigia magoti na kumsihi asitishe azma yake hiyo, ambayo alikubali kuendelea na uongozi hadi juzi Jumamosi alipoijulisha rasmi kamati yake ya utendaji kuwa ni muda muafaka kwa yeye kukaa pembeni.

"Nia yangu yakujiuzulu ni ya muda mrefu, sikutaka kufanya maamuzi katikati ya ligi ningewachanganya wachezaji, nashukuru tumetetea ubingwa wetu naiacha Yanga ikiwa na kikosi bora na hata makocha pia.

" Yapo mengi mazuri ninayojivunia Yanga ikiwemo umoja na mshikamano, ikumbukwe nilingia wakati kuna mgogoro mkubwa, nikafanikiwa kumaliza hivyo ni muda sahihi na muafaka kwa Mimi kukaa pembeni.

Ikumbukwe Yanga ni klabu ya wanachama, Yanga ni kubwa kuliko mtu yoyote, naamini watakaofuatia wataendeleza pale nilipoishia, " alisisitiza.

Kwa upande wa Katibu wa Yanga Charles Mkwasa akizungumzia hilo alisema "Nimeona taarifa ya Mwenyekiti wetu kwenye mitandao, na nilikuwa nawasiliana naye kila siku kwa email na hajawahi kunieleza hili, ila kama kweli ni maamuzi yake basi tutayaheshimu," alisema.


Hatahivyo, kuondoka kwa Manji kunaweza kukawa si pigo sana kwa klabu hiyo ya Jangwani ambayo tayari imesaini mamilioni ya fedha kwa kudhaminiwa na Sports Pesa huku ikielezwa kuwa kuna makampuni kadhaa ambayo yapo mbioni kudhamini timu hiyo ya mtaa wa Twinga na Jangwani.

No comments:

Post a Comment