Friday, 1 April 2016

Riadha Tanzania watangaza wachezaji kuunda timu ya taifa ya U-20 itakayopiga kambi kwa Filbert Mkuza Kibaha


Baadhi ya wanariadha chipukizi wa Tanzania wakichuana katika moja ya mashindano kwenye Uwanja wa Taifa hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
RIADHA Tanzania (RT) imetangaza majina 27 ya timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 kwa ajili ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yatakayofanyika nchini Aprili 29 na 30.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo Robert Kalyae, timu hiyo ya wanawake na wanaume ambayo itapiga kambi katika shule za Filbert Bayi Mkuza Kibaha, imechaguliwa baada ya kufanyika mashindano ya mchujo mara tatu.

Alisema kuwa mashindano hayo ya mchujo yaliyofanyika Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

Timu ya wanaume inaundwa na Adinani Haruna wa Moshi atakayeshiriki mbio za mita 100 na 200, Benjamin Michael wa Dar es Salaam atakayeshiriki mbio za mita 100 na 200, Oscar Prosper (Moshi) atakayekimbia mbio za mita 400.

Wengine ni Imani James na John Silima wa Dar es Salaam watakimbia mbio za mita 400, Thobias Bula, Simon Francis, Emmanuel Gadiye na Francis Dambel kutoka Karatu watakimbia mita 800 na 1500.
Wachezaji na viongozi wa timu ya mkoa wa Dar es Salaam katika picha ya pamoja baada ya kushiriki mashindano ya taifa mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kalyae aliwataja wachezaji wengi wa timu hiyo kuwa ni pamoja na Elisha Wema wa Manyara na Jackson Makombe wa Pwani mita 5,000.

Watakaorusha mkuki, kisahani na tufe ni pamoja na Sabas Daniel wa Bagamoyo, kuruka chini ni Anthony Mwanga, anayesoma Afrika Kusini, Dennis David wa Arusha, Hafidh Khalfan mita 400 na 800, na Jimmy Kisumo wa shule ya sekondari Tambaza ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa wanawake waunaokimbia mbio za mita 100 na 200 ni Rehema John toka Magu, Jane Maiga wa Pwani, (mita 400 na kuruka chini) watakuwa Hynes Bamopenja wa Dar es Salaam na Rose Seif wa Pwani.

Watakokimbia mita 800 na 1500 ni pamoja na Dorcas Boniface, Regina Deogratius, Betrina Michael na Easter Martin, Angelina Tsere mita 5,000 na Aisha Mohamed mita 5,000.
Mbali na Kalyae makocha wengine watakaoinoa timu hiyo ni pamoja na Mwinga Mwanjala na Ephania Mugaza wakati daktari ni Richard Yomba na meneja wa timu hiyo ni Peter Mwita.

Alisema vigezo walivyotumia kuchagua timu hiyo ni pamoja na kuzingatia muda wa wachezaji katika mashindano hayo ya majaribio, umri pamoja na bidii na kujituma.

1 comment: