Sunday 24 April 2016

Papa Wemba afariki jukwaani akitumbuiza Abidjan, Ivory Coast



Na Mwandishi Wetu
GWIJI wa muziki wa Kikongo, Papa Wemba (pichani) anayejulikana kwa majina mengi yakiwemo King of Rhumba Rock, amefariki dunia baada ya kuanguka jukwaani wakati akitumbuiza jijini Abidjan, Ivory Coast.

Papa Wemba ni mmoja wa wanamuziki waliochangia kukua kwa muziki wa Afrika na pia wanamuziki wengi wakubwa wamepita mikononi mwake.

Mpaka mauti yanamkuta alikuwa na umri wa miaka 66, video ya tukio inaonyesha alianguka ghafla wakati wacheza shoo wake wakiwa mbele ya jukwaa na waliendelea kucheza kwa hatua kadhaa kabla ya kusitisha na kwenda kumuangalia akiwa chini.

Inaelezwa kuwa tukio la kuanguka lilitokea mara baada ya Papa Wemba kuimba wimbo wake wa tatu jukwaani hapo.

Kituo cha redio cha Okapi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kilitangaza juu ya kifo hicho, lakini hakikusema sababu haswa zilizoondoa roho ya mkongwe huyo.
 
Marehemu ambaye jjina lake halisi ni Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba alikuwa kitumbuiza kwenye Tamasha la Urban Music Festival

Papa Wemba
Kuzaliwa: Juni 14, 1949
Kufariki: Aprili 24, 2016
Aina ya muziki aliokuwa akiimba: Soukous, Rhumba.

No comments:

Post a Comment