Wednesday, 27 April 2016

Marwa, Failuna washinda Heart marathon 2016


Wanariadha wa mbio za kilometa 21 wakijiandaa kwa mbio hizo za Heart Marathon kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
DICKSON Marwa na Failula Abdul jana walishinda Heart Marathon, mbio zilizoanzia na kumalizikia kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani.

Katika mbio hizo za kilometa 21, Marwa wa Dar es Salaam aliibuka wa kwanza kwa upande wa wanaume kwa kutumia saa 1:10.42 wakati Abdul wa Arusha aliwashinda wanawake wenzake kwa kutumia saa 1:20.31, ambapo kila mmoja alipata Sh 500,000. 

Washindi wa pili na tatu kwa wanaume ni Panuel Mkungo na Eric Mombo wote wa Holili, Rombo mkoani Kilimanjaro waliomaliza kwa saa 1:11.88 na 1:13.46. 


Wakimbiaji wa kilometa tano wakijiandaa kabla ya kuanza kwa mbio hizo.
Akizungumza kabla ya kutoa zawadi kwa washindi, mgeni rasmi wa mbio hizo ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Michezo nchini, Alex Nkeyenge amewataka Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.


Alisema asilimia kubwa ya Watanzania wamekuwa wakiendelea kusumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza  kutokana na wengi wao kutokuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi.  

"Michezo ni afya pamoja na ajira kama tunataka kuona magonjwa haya yanatoweka kabisa nchini, basi tujenge utamaduni wa kufanya mazoezi pamoja na kubadili mitindo yetu ya maisha, alisema Nkeyenge. 

Aidha, alisema Serikali imeahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa waandaaji wote wa mashindano yoyote endapo watahitaji msaada.  Hakuna Serikali isiyopenda michezo niseme tu Serikali ipo bega kwa bega na nyinyi na wale wote watakaokuwa wakianzisha mashindano yoyote, aliongeza Nkeyenge. 

Pia ametoa mwito kwa washiriki wote wa Heart Marathon pamoja na washindi kuhakikisha wanaendeleza vipaji vyao vya mbio na wale wote walioshindwa wasikate tamaa. 

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Heart Marathon, Dk Chakou Khalfan amewashukuru washiriki wote na kuahidi kuhakikisha mbio hizo zinakuwa na muendelezo mwaka hadi mwaka na kuenea nchi nzima, lengo likiwa ni kuwajengea Watanzania utamaduni wa kupenda mazoezi pamoja na kuwajenga wakimbiaji ili waweze kushiriki mashindano hata ya kimataifa.

Alisema mashindano hayo yamegawanya kwa kilometa ambapo mbio ndefu zilikuwa zile za kilometa 21, 10, tano, meta 700 na zile za watoto wadogo za meta 50. 

Aidha, mashindano hayo pia yalitoa fursa kwa washiriki kupima afya zao bure ikiwemo kuangalia magonjwa mbalimbali hasa yale yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na mengineyo. 

Katika mbio za baiskeli za matairi matatu za walemavu, Mohammed Abdallah wa Dar es Salaam aliibuka wa kwanza kwa kutumia dakika 38.12 huku,Simon Mulewa aliibuka wa pili kwa dakika 39.10 na Romanus Nyambulage alimaliza wa tatu kwa kutumia dakika 45.15.

No comments:

Post a Comment