Wednesday 27 April 2016

Wachezaji Uchukuzi SC waibiwa gesti Dodoma katika mashindano ya Mei Mosi




Kocha Rose Mkisi akihamasisha timu yake ya kuvuta kamba ya wanaume ya TPDC walipocheza na Ukaguzi katika michuano ya Mei Mosi. TPDC walishinda kwa mivuto 2-0.

Na Mwandishi Wetu
WACHEZAJI wa timu ya Uchukuzi SC inayoshiriki kwenye mashindano ya Mei Mosi mkoani hapa, juzi wameibiwa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 1.5 katika nyumba ya kulala wageni waliyofikia ya MT iliyopo Chadulu mjini hapa. 

Mkuu wa Upelelezi wa wilaya, Charles Chalula, alipoulizwa juu ya tukio hilo jana alikiri taarifa kufika ofisini kwake, na tayari jeshi hilo linawashikilia watu watatu akiwemo mhudumu wa hoteli hiyo.

Pia alisema atawasiliana na mkurugenzi wa hoteli hiyo, aliyemtaja kwa jina moja la Haule ili aweze kurudisha fedha za wachezaji, ambazo walilipa kukaa hapo hadi Mei 2 mwaka huu michezo itakapokamilika. 

"Ni kweli wachezaji wamekuwa na hofu na usalama wao na mali zao, nitamtafuta mmiliki wake akiwezekana arudishe fedha zao leo hii hii (jana) ili waweze kuhamia hoteli nyingine, ila nitahakikisha suala la upelelezi tunalifanya haraka ili hivi vitu vilivyoibwa vipatikane haraka, alisema Chalula. 

Timu ya kamba ya wanaume ya Ukaguzi wakivutana na wenzao wa TPDC, lakini walishindwa kwa mivuto 2-0.
Kwa mujibu wa taarifa ilizonazo gazeti hili, wizi huo ulitokea majira ya saa 10:00 jioni wakati wengi wa wachezaji hao wakiwa Uwanja wa Jamhuri kuishangilia timu ya soka soka iliyokuwa inapambana na CDA ya hapa. Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Mbali ya soka, wachezaji wengine wa Uchukuzi ni wa michezo ya kuvuta kamba, bao, drafti na karata. Mmoja wa wachezaji hao, Ally Suleiman katika chumba chake ameibiwa kompyuta mpakato yenye thamani ya Sh milioni 1.2, fedha taslimu Sh 120,000 na mashine inayohifadhia nyaraka mbalimbali yenye thamani ya Sh 180,000.

Thea Samjela wa Uchukuzi SC (kuilia) akichuana na Regina Mutimangi wa TPDC katika mchezo wa bao.
Suleiman aliyefungua kesi ya wizi iliyopewa jalada namba IR/3844/2016 pia aliibiwa vitu mbalimbali ikiwemo kadi ya Bima ya Afya na leseni ya udereva. Mchezaji mwingine, Tracius Dionis alisema wezi hao waliingia chumbani kwake na kutawanya vitu kwenye begi lake, lakini hawakuiba chochote zaidi ya kuchukua seti ya televisheni, mali ya nyumba hiyo ya kulala wageni.

Aliongeza kuwa, walifungua chumba cha mchezaji mwingine, Aminiel Ombeni ambaye amesafiri kwenda Moshi kuzika baada ya kupata msiba wa mama yake, na bado haijajulikana vilivyoibwa kwani begi lake lilikutwa katika  chumba cha mteja aliyefika juzi mchana.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya Uchukuzi, Alex Temba alisema wamesikitishwa na tukio hilo kwani haijawahi kutokea katika mikoa yote waliyowahi kushiriki michezo ya Mei Mosi.


Neema Makassy  wa Uchukuzi SC (kulia) akitafakari katika mchezo wa bao dhidi ya Joyce Kimondi wa Ujenzi.
Temba aliomba jeshi la polisi kuonyesha ushirikiano kama lilivyoahidi siku ya kwanza timu ziliporipoti mkoani hapa kuwa watatoa ulinzi mkubwa, basi watekeleze ahadi yao kutokana na wachezaji wote ni wageni mkoani hapa.

"Suala hili limetusikitisha sana huyu ni mfanyakazi mwenzetu pamoja na kwamba tupo katika suala la michezo lakini aliendelea na kazi za ofisi na jana tu alikuwa akituma taarifa mbalimbali, basi tunawaomba polisi watusaidie hivi vitu vipatikane, na hata waongeze ulinzi kwani ni tukio la aibu kuwaibia wageni, alisema Temba.

No comments:

Post a Comment