Tuesday, 5 April 2016

Yaya Toure kuondoka Man City kumkwepa kocha Guardiola anayetua mwishoni mwa msimuLONDON, England
KIUNGO wa Manchester City Yaya Toure ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu baada ya hadi sasa kutopewa mkataba mpya, amesema wakala wake.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast, na ni mchezaji bora wa mwaka wa Afrika mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2011, alijiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu akitokea Barcelona kwa pauni milioni 24 Julai mwaka 2010.

Miaka sita iliyopita Toure aliuzwa na aliyekuwa kocha wa Barca Pep Guardiola, ambaye sasa anatua Man City kuchukua nafasi ya Manuel Pellegrini wakati Mhispania huyo atakapoondoka Bayern Munich mwishoni mwa msimu.

"Tulisubiri kwa muda mrefu. Manchester City iliahidi kuongeza mkataba lakini hakuna kilichofanyika hadi sasa, hivyo Yaya ataondoka Juni, alisema wakala wake Dimitri Seluk.

"Bila shaka hilo litakuwa limesikitisha sana Yaya, lakini ni mchezaji wa kulipwa atabaki katika mataba na ataendelea kuifanyia mazuri Man City katika kipindi kilichobaki.

Vyombo vya habari vimekuwa vikimuhusisha Toure na kutaka kuhamia Inter Milan inayofundishwa na kocha wazamani wa Man City Roberto Mancini.

"Ofa kibao zimekuja zikitaka kumsajili Yaya na tunazichambua, alisema Seluk. "Inter? Tunazungumzia kuhusu klabu kubwa.

"Kila mmoja anajua kuhusu uhusiano kati ya Yaya na Mancini lakini...bado hatujafanya uamuzi wowote.

Toure alishinda taji la Ligi Kuu ya England akiwa na Man City mwaka 2012 na 2014, Kombe la FA mwaka 2011 na lile la ligi mwaka 2014 na 2016.

Man City leo watakuwa wageni wa Paris St Germain katika mchezo wa kwanza wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

No comments:

Post a Comment