Wednesday 6 April 2016

Al Ahly yatua na kikosi cha wachezaji 21 tayari kuivaa Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa



Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Al Ahly ya Misri imetua nchini leo alfajiri tayari kwa pambano lao la Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Yanga litakalofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Pambano hilo ni la hatua ya 16 bora, ambapo timu hizo zitarudiana siku 10 zijazo nchini Misri ili kusaka timu itakayotinga hatua ya makundi.

Timu hiyo imekuja na wachezaji wakali 21 pamoja na kocha wao Martin Jol, ambaye alianza kuifundisha timu hiyo mwezi uliopita baada ya kumwaga wino.

Kocha wa Al Alhy, MMartin Jol mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere leo alfajiri.
Kocha huyo wa Ahly amewaita wachezaji wake wote wakali ambao wamo katika safari hiyo.

Pambano hilo linakumbushia lile la mwaka 2014, ambapo Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Ahly kabla ya kufungwa bao kama hilo na kufanya mchezo huo kuamliwa kwa matuta, ambapo Yanga ilifungwa 4-3.

Said Bahanuzi na Mbuyi Twitte ndio walioikosesha Yanga ushindi baada ya kukosa penalti zao katika mchezo huo uliofanyika jijini Cairo, Misri.

Katika kikosi hicho, Jol amewaacha beki Mohamed Naguib, kiungo Saleh Gomaa na Ahmed Hamdy, ambacho kimetua leo tayari kwa mchezo huo.

Mchezaji aliyepona hivi karibuni misuli, Sherif Ekramy ameitwa baada ya kuwa nje ya uwanja tangu Februari,pamoja na kipa wa akiba Ahmed Adel akichukua nafasi katika mechi zilizopita.

Al Ahly imetinga hatua ya 16 bora baada ya kuifungisha virago Recreativo ya Angola kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-0, wakati Yanga walipinya baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

Yanga walishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Amavubi jijini Kigali, Rwanda kabla ya kutoka sare ya kufungana 1-1 katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Ahly:

Makipa: Sherif Ekramy, Ahmed Adel na Mosad Awad.

Mabeki: Ahmed Fathi, Bassem Ali, Mohamed Hani, Saad Samir, Rami Rabia, Ahmed Hagazy na Sabri Rahil.

Viungo: Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Amr El-Sulaya, Ahmed El-Sheikh, Walid Soliman, Moemen Zakareya, Ramadan Sobhi na Abdalla El-Said.

Washambuliaji: Malick Evouna, Amr Gamal na Emad Meteb.
Yanga wenyewe wako Chake Chake Pemba wakijifua kwa ajili ya pambano hilo linalotarajiwa kuwa kali na la kuvutia huku Al Ahly wakitaka kuendeleza makali yao na Yanga kulipa kisasi cha kutolewa mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment