Wednesday, 13 April 2016

Kumbe Barcelona inafungika! yachapwa na kuvuliwa ubingwa wa Ulaya, Bayern Munich yasonga mbele kwa mbinde


Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akiwa hoi wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Club Atletico de Madrid uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Vicente Calderon jijini Madrid, Hispania. Barcelona ililambwa 2-0.

 MADRID, Hispania
BARCELONA imevuliwa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 2-0 na Atletico Madrid, zote za Hispania usiku wa kuamkia leo katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Vicente Calderon mjini Madrid.

Atletico Madrid wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya awali kufungwa 2-1 Uwanja wa Camp Nou, Barcelona.

Mabao yote ya timu ya Muargentina Diego Simione leo yamefungwa na Antoine Griezmann dakika ya 36 na lingine kwa penalti dakika ya 88.

Bayern Munich imefakiwa kwa mbinde kwenda Nusu Fainali baada ya kuitoa Benfica kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya sare ya 2-2 leo Uwanja wa Luz.

Mabao ya Benfica yamefungwa na Raul Alonso Jimenez Rodriguez dakika ya 27 na Anderson Souza Conceicao dakika ya 76, wakati ya Bayern iliyoshnda 1-0 katika mchezo wa kwanza nyumbani wiki iliyopita, yamefungwa na Arturo Vidal dakika ya 38 na Thomas Muller dakika ya 52.


Mshambuliaji Mfaransa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann (aliyebebwa) akishangilia bao pamoja na kiungo wa timu hiyo Gabi wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya juzi.

Atletico Madrid na Bayern Munich zinaungana na Real Madrid ya Hispania na Manchester City ya England katika Nusu Fainali, ambayo droo yake itapangwa Ijumaa.


Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro aliipeleka Real Madrid Nusu Fainali juzi kwa mara ya sita mfululizo baada ya kufunga mabao matatu peke yake au hat-trick, ikishinda 3-0 Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid dhidi ya Wolfsburg ya Ujerumani.

Real imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa 2-0 Ujerumani na Ronaldo alifunga mabao yake katika dakika za 15, 17 na 77 na kufikisha mabao 46 msimu huu kwenye mashindano yote.

Kevin de Bruyne naye alifunga bao pekee dakika ya 14 Uwanja wa Etihad jana na kuipeleka Manchester Nusu Fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya PSG.

Man City imesonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2 baada ya wiki iliyopita kulazimisha sare ya 2-2 mjini Paris. 

Ushindi huo unamfanta kocha Manuel Pellegrini kuweza kukutana na mrithi wake mwishoni mwa msimu, Pep Guardiola baada ya Bayern Munich pia kuingia hatua hiyo ya Nusu Fainali.

No comments:

Post a Comment