Saturday 16 April 2016

Maghembe ashuhudia rekodi ya Ngorongoro Marathon ikivunjwa na mwanariadha wa taifa, Ismail Juma baada ya kuwagalagaza wenzake kwa dakika nne zaidi



Wanafunzi wavulana wa shule za sekondari wakianza mbio za kilomita 2.5 za Ngorongoro Marathon mjini Karatu leo.


Na Mwandishi Wetu, Karatu
MBIO za tisa za Ngorongoro Marathon zimefanyika jana huku mwanariadha wa taifa Ismail Juma akivunja rekodi ya mbio hizo kwa kutumia saa 1:02.48 na kuipiku ile ya awali ya saa 1:03.00 iliyowekwa miaka mingi iliyopita.

Juma tangu mwanzo wa mbio hizo alionesha kila dalili ya kuibuka na ushindi tena mnono baada ya kuwaacha wenzake kwa mbali na kumaliza wa kwanza na kushinda mshindi wa pili kwa dakika nne zaidi, kitu ambacho ni nadra sana kutokea katika mbio zozote.

Wanafunzi wakichuana katika mbio za kilometa 2.5 za Ngorongoro Marathon mjini Karatu leo.
Mbio hizo zilianzishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye baadae alishuhudia Juma akivunja rekodi ya mbio hizo zilizoanzia katika lango la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia kwenye viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.

Baada ya kukimbia katika kundi moja na wenzake kwa karibu kilomita nne, Juma aliwaacha kuanzia hapo hadi mwisho wa mbio huku wenzake wakibaki wakisoma namba.

Washiriki wa mbio za kilometa 21 za Ngorongoro Marathoni wakijiandaa kwa mbio hizo leo katika lango la kuingilia na kutokea Hifadhi ya Ngorongoro.
Juma alimzidi mshindi wa pili kwa takribani dakika nne baada ya Stephen Uche kumaliza mbio hizo kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu akitumia saa 1:06.3 huku Yohana Elisante akishika nafasi ya tatu kwa saa 1:06.24.

Mwanariadha huyo ni miongoni mwa wanariadha wanaounda timu ya taifa inayotarajia kushiriki Michezo ya 31 ya Olimpiki itakayofanyika baadae mwaka huu Rio, Brazil na atakimbia mbio za mita 5,000 na 10,000 endapo atafuzu.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (watatu kutoka kushoto mbele) akipewa maelekezo kabla hajaanzisha mbio za nusu marathoni za Ngorongoro leo katika lango la kuingilia na kutokea katika hifadhi ya Ngonrongoro.
Kwa upande wa wanawake, Fainuna Abdi ameendelea kuwaburuza wakongwe baada ya kuibuka wa kwanza katika mbio hizo kwa kutumia saa 1:11.52 na kumzidi mchezaji wa timu ya taifa Nathalia Elisante aliyemaliza wa pili kwa kutumia saa 1:15.46 huku Fadhila Tipa akiwa wa tatu kwa saa 1:16.54.

Kocha wa timu ya taifa ya Ridha inayojiandaa kwa Michezo ya Olimpiki iliyopiga kambi West Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro, Francis John akizungumza kwa njia ya simu jana alisema Juma alistahili kushinda kwani yuko vizuri kutokana na mazoezi aliyofanya.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akianzisha mbio za tisa za Ngorongoro leo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Omary Qwang na kushoto ni Mama Zara.
Alisema hata kabla ya mbio alimuahidi kocha wake kuwakimbiza wenzake hadi watu washangae, na ni kitu ambacho amekifanya jana kwa kuwaacha wenzake mbali.

Naye Juma akizungumza baada ya kumaliza mbio hizo alisema siri ya mafaniki yake ni mazoezi ya muda mrefu anayoendelea kufanya katika kambi ya timu ya taifa.

Naye Maghembe alisema anataka mbio za 10 za Ngorongoro ziwe za kimataifa zaidi kwa kutoa wanariadha watakashiriki na kushinda katika marathoni za kimataifa kama zile za London, New York, Boston na zingine.

Kwa miaka mingi sasa wanariadha wa Tanzania wameshindwa kabisa kushiriki katika mbio kubwa za kimatiafa kutokana na kuwa na viwango vidogo, ambavyo haviwawezeshe kushiriki tofauti na miaka ya nyuma.

Wanariadha kama akina Juma Ikangaa, Francis Nade, Zebedayo Bayo, Simon Mrashani, Lwiza John, Francis Naali na wengine wengi walishiriki mbio mbalimbali kubwa za mialiko kutokana na kuwa na muda mzuri kimataifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Omary Qwaang alisema kuwa vijana waendelee kujiweka fiti ili waweze kufanya vizuri katika mbio hizo na zingine na kulipatia sifa taifa.

Alisema kuwa mashindano ya Ngorongoro yanawapa matumaini makubwa ya wanariadha wetu kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya kimataifa.

Mbio hizo za tisa za Ngorongoro zimefanyika huku huku kukiwa na mvua kubwa iliyoanza kunyesha tangu juzi na kuendelea siku nzima ya jana.

Mbali na mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, pia kulikuwepo mbio za kilometa tano kwa ajili ya makampuni na taasisi mbalimbali pamoja na zile za kilomita 2.5, ambazo ziliwashirikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Mbio za mwaka huu zimedhaminiwa na Zara Charity pamoja na Zara Tours, Bonite Bottlers, Malenga Investment, Exim Bank, Equity Insurance, Davis Mosha na African Safari.   

No comments:

Post a Comment