Friday, 21 April 2017

Real Madrid kuivaa Atletico Madrid, Juventus wapangwa na Monaco Ligi Mabingwa Ulaya

Real Madrid walipotwaa ubingwa wa Ulaya baada ya kuifunga Atletico Madrid mwaka jana.
ZURICH, Uswisi
MABINGWA watetezi Real Madrid watakabiliana na wapinzani wao wakubwa Atletico Madrid katika nusu fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, wakikumbushia fainali ya mwaka jana.

Kikosi hicho cha Zinedine Zidane kinaweza kuwa klabu ya kwanza kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Ulay katika fainali itakayopigwa Juni 3 kwenye Uwanja wa Cardiff.

Klabu ya Ufaransa ya Monaco itacheza na Juventus ya Italia katika mchezo mwingine wa hatua hiyo ya nne bora.

Mechi za kwanza za nusu fainali zitapigwa Mei 2 na 3, huku zile za marudiano itafanyika wiki inayofuata.

Real, ina lengo la kutwaa tena taji kubwa Ulaya ikiwa watafanikia itakuwa ni mara yao ya 12, baada ya kuifunga mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-3 na kutinga nusu fainali.

Wakati huohuo, Atletico Madrid ilimaliza ubabe wa mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Leicester kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya mechi zote mbili.

Juventus iliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Barcelona huku Monaco ikiondosha Borussia Dortmund 6-3.

No comments:

Post a Comment