Friday 14 April 2017

Arsenal yavunja benki kumbakisha Alexis Sanchez sasa atalipwa sh Milioni 838 kwa wiki

LONDON, England
KLABU ya Arsenal hatimaye imeufyata baada ya kuamua kuvunja benki na kuahidi kumlipa Alexis Sanchez kiasi cha pauni 300,000 (sawa na sh Milioni 838) kama mshahara wa mchezaji huyo kwa wiki.

Gazeti la Standard Sport lilibainisha Desemba kuwa, mchezaji huyo mwenye uimri wa miaka 28, alikuwa akitikisa kiberiti ili alipwe mshahara mnono kama ule wa Mfaransa wa Manchester United, Paul Pogba wa pauni 290,000 (sawa na sh Milioni 810) kwa wiki.

Habari zilizopatikana kutoka Arsenal zinasema kuwa kwa sasa the Gunners imeonesha dalili za kutaka kutoa kiasi hicho cha fedha ili kumbakisha mchezaji huyo katika klabu hiyo.

Manchester City, Chelsea na Paris St Germain wanatarajia kuweka mezani ofa kwa ajili ya kumtaka mchezaji huyo mwishoni mwa msimu huku Arsenal ikitaka ilipwe kiasi cha pauni Milioni 50 kama itashindwa kufikia makubaliano na mchezaji huyo.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile katika wiki za hivi karibuni amechanganyikiwa zaidi wakati Arsenal ikipoteza mechi saba kati ya 12 katika mashindano yote huku mashabiki wakimtaka kocha Arsene Wenger kuachia ngazi mara moja mwishoni mwa msimu.


Mesut Ozil ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa sasa Arsenal akiweka kibindoni kiasi cha pauni 140,000 — Sanchez anapata pauni 130,000 — lakini klabu inajua madhara ya kuwapoteza wachezaji bora kwa wapinzani wao wakubwa.

No comments:

Post a Comment