Tuesday 25 April 2017

Benitez kupewa fungu zaidi la usajili baada ya kuipandisha Newcastle United hadi Ligi Kuu

LONDON, England
KOCHA wa Newcastle Rafael Benitez (Pichani),  anatakiwa kupewa fedha ili kuimarisha kikosi chake kabla ya timu hiyo haijaanza msimu mpya katika Ligi Kuu, anasema gwiji wa klabu hiyo, Alan Shearer.

Benitez alitumia zaidi ya kiasi cha pauni Milioni 50 katika kipindi kilichopita cha majira ya joto baada ya timu hiyo kushushwa daraja, lakini Shearer anasema kuwa kuna hatari ya kumkosa kocha huyo Mhispania, endapo hatapewa fedha zaidi.

"Nafikiri kama atapewa fungu zaidi la usajili bila shaka kitakuwa kishawishi kikubwa kwake kubaki katika timu hiyo, “alisema mchezaji huyo mwenye rekodi ya kufunga mabao mengi katika timu hiyo.

Newcastle ilipanda daraja baada ya kushinda mabao 4-1 katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Preston uliofanyika Jumatatu.

Nahodha huyo wazamani wa England aliongeza: "Ni mtu mkubwa katika klabu. Anapapenda mahali hapa na ni mvumilivu na muhimu zaidi ni kwa Newcastle kuendelea kumbakisha.
"Nina uhakika atataka timu iimarishwe na atataka hilo lifanyike.”

"Watu wamebaini kuwa timu inahitaji kuimarishwa zaidi ili kufikia pale wanapotaka kuwa, katika nusu ya juu ya Ligi Kuu.

"Sasa ni mahali ambako Newcastle inataka kuwa, kuwa katika Ligi Kuu na hawataki kuwa katika nafasi tatu za chini, ambazo ni za kupambana dhidi ya kushuka daraja.”

Winga wazamani wa Newcastle, Chris Waddle naye aliunga mkono maneno ya Shearer, ambapo anaamini kuwa, Benitez atataka kuimarisha kikosi chake ili kifanye vizuri.


Benitez aliteuliwa kuifundisha Newcastle Machi 2016 lakini alishindwa kuiokoa timu hiyo kuteremka daraja hadi daraja la kwanza.

No comments:

Post a Comment