Friday, 21 April 2017

Ukata waitoa Polisi Moro netiboli Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Polisi Morogoro nayo imetangaza kutoshiriki katika mashindano ya netiboli ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia keshokutwa Jumapili hadi Aprili 30.

Polisi ni timu ya timu ya Tanzania Bara kujitoa baada ya washindi wa pili Uhamiaji kutangaza mapema kujitoa kwa sababu kama hizo.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Annie Kibira (Pichani) alisema jana kuwa, Polisi imethibitisha leo kuwa haitashiriki katika mashindano hayo kwa sababu ya ukata.

Alisema kwa Bara timu pekee yenye uhakika wa kushiriki mashindano hayo ni Jeshi Stars na inatarajia kuondoka kesho Jumapili kwenda Nairobi.

Wakati huohuo, timu za Zanzibar zilitarajia kuanza safari jana ya kwenda Nairobi kupitia jijini Dar es Salaam, ambako wataondoka leo pamoja na viongozi wanne wa Chaneta.

Timu ya Jesho la Kujenga Uchumi, JKU, itakuwa na wachezaji 12 wakike na 12 wakiume na viongozi watano kushiriki mashindano hayo.

Timu nyingine ya Zanzibar itakayoshiriki mashindano hayo ni ile ya KVZ.


Mbali na Kibira, kiongozi mwingine wa Chaneta ni kaimu katibu mkuu, Hilda Mwakatobe wakati waamuzi ni Eliakimu Christopher na Jenny Butinini.

No comments:

Post a Comment