Sunday, 16 April 2017

Savio yaendelea kuchanja mbuga, ABC ikiidadabua Don Bosco 73-50 Ligi ya Kikapu RBA Dar es Salaam


Na Mwandishi Wetu

SAVIO imeendelea kuongoza katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam ya RBA inayoendelea kushika kasi.

Baada ya mechi za jana kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa, ambapo ABC iliifunga Don Bosco kwa pointi 73-50 huku Oilers wakiitambia Chui kwa pointi 68-50, Savio wako kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 22.

Vijana au City Bulls wenyewe wako katika nafasi ya pili kwa pointi 21 huku Ukonga Kids wakifuatia katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 19 huku JKT wakiangukia katika nafasi ya nne.

Wakongwe Pazi wenyewe wako katika nafasi ya tano baada ya kujikusanyia poiti 17, Kurasini nao wana pointi 17 lakini wako katika nafasi ya sita, Mabibo Bullet wenyewe wako katika nafasi ya saba.

Mkurugenzi wa Ufundi na Mashindano wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, Halleluya Kavalambi alisema kuwa ABC, Jogoo, UDSM Outsiders na Olilers wanashika nafasi ya nane hadi 10.

Wakati huohuo, Kavalambi alisema kuwa viporo vya baadhi ya mechi vitapigwa Jumatano, ambapo ABC watacheza na Tanzania Prisons saa 10:00 Jioni, huku Jogoo wataoneshana kazi na Mgulani kuanzia saa 12 jioni na Pazi atakwaruzana na Chui kuanzia sasa 2 usiku.

No comments:

Post a Comment