Friday, 14 April 2017

Uchukuzi Sports Club watamba kutoa kichapo kwa kila watakayekutana naye Mei Mosi Moshi

Wachezaji wa timu ya Uchukuzi Sports Club wa timu ya Kuvuta Kamba wakijifua kwa ajili ya mashindano ya Mei Mosi.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Uchukuzi Sports imetamba kutetea mataji yake na kuongeza mengine katika mashindano ya Mei Mosi yatakayofanyika kuanzia wiki ijayo mjini Moshi.

Katibu wa Michezo wa Uchukuzi Sports Club, Alex Temba alisema juzi wakati wa mazoezi ya timu hiyo kuwa, wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanatetea mataji waliyonayo na kuongeza mengine.
Timu ya soka ya Uchukuzi wakati wa mapumziko walipocheza jana dhidi ya Kitunda FC na kutoka sare ya bila kufungana.
Akifafanua, Temba alisema kuwa Uchukuzi Sports ndio mabingwa wa jumla wa mashindano hayo ya wafanyakazi, ambao waliutwaa mwaka jana mjini Dodoma na kukabidhia Kombe na Rais Dk John Pombe Magufuli.

Alisema wanakwenda Moshi kutetea mataji ya soka, kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, mbio ndefu kwa wanaume na wanawake, baiskeli kwa pande zote mbili pamoja na michezo ya jadi ya bao, karata na drafti.
Timu ya netiboli wakijfua.
Alisema kuwa maandalizi yao ambayo walianza muda mrefu, yanaendelea vizuri na wanatarajia kuondoka wiki ijayo kwenda Moshi tayari kwa mashindano hayo.

Timu ya Uchukuzi Sports inaundwa na wachezaji kutoka taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Naye nahodha wa timu hiyo, Toba Ally alisema kuwa hawana wasiwasi, kwani wana uhakika maandalizi yao mazuri kuwanyoa wapinzani wao katika michezo yote.


Alisema mwaka jana walitwaa vikombe vitano, lakini mwaka huu watabeba mataji zaidi, kwani maandalizi yao ndio yanawafanya kujiamini kiasi hicho.

No comments:

Post a Comment