Tuesday 25 April 2017

Prisons yaitoa jasho Makongo wavu wa Muungano

Wachezaji wa Tanzania Prisons (kushoto) wakichuana na wale wa Makocha Sekondari wakati wa mchezo wa mpira wa wavu wa Muungano leo kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Magereza ilishinda kwa seti 3-0.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Tanzania Prisons leo  ilimeichapa Shule ya Sekondari ya Makongo wanawake kwa seti 3-0 katika mchezo wa mashindano ya Muungano ya mpira wa wavu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wa Tanzania Prisons (kulia) wakichuana na wale wa Makocha Sekondari wakati wa mchezo wa mpira wa wavu wa Muungano leo kwenye Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Makongo imekutana na kipigo hicho ikiwa ni siku moja tu baada ya kuifunga Jeshi Stars ambaye ni bingwa mtetezi kwa seti 3-1.
Katika mchezo huo, Tanzania Prisons ilishinda 25-20 katika seti ya kwanza,kabla ya kuibuka na 25-23 katika seti ya pili huku katika seti ya mwisho ikitamba kwa pointi 25-17.

Kwa upande wa wanaume, Kinyerezi iliifunga Mjimwema kwa seti 3-0, ambapo washindi walifanya kweli kwa ushindi wa 28-26, 25-22 na 25-20.
Akizungumza kando ya mashindano hayo, Katibu Msaidizi wa Chama cha mchezo wa Wavu Tanzania, (TAVA) Alfred Selengia alisema mashindano hayo yana ushindani tofauti na mwaka jana.

“Mashindano yanaendelea vizuri na ushindani ni mkubwa tofauti na mwaka jana. Bingwa atapata kombe na medali pamoja na mshindi wa pili,” alisema Selengia.

Pia Selengia alisema bingwa ndiye atawakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika yatakayofanyika mwakani kwa timu za wanawake na wanaume.
Timu zinazoshiriki ni bingwa mtetezi Jeshi Stars, Chui, Polisi Zanzibar, Moro Stars, Makongo Sekondari, Tanzania Prisons, Saut Mwanza, Mafunzo ya Zanzibar, Dodoma, Mjimwema, Victory Sports na Kinyerezi.

Timu za wanawake ni pamoja na Tanzania Prisons, Jeshi Stars, Shule ya Sekondari ya Makongo, Saut ya Mwanza, Mjimwema na Dodoma.

No comments:

Post a Comment