Monday 24 April 2017

Simbu apongezwa kung'ara London Marathon

Balozi wa DStv na Mshiriki pekee kutoka Tanzania aliyeshiriki mashindano ya London Marathon yaliyofanyika jana jijini London Alphonce Simbu  ameibuka mshindi wa tano huku akivunja rikodi yake kwa kutumia muda wa 2:09.10 ambao ndio muda wake bora zaidi tangu aanze kushiriki mashindano ya kimataifa.

 Kabla ya hapo rekodi yake ilikuwa muda wa 2:09.21 aliyoiweka mwaka jana kwenye mashindano ya Lake Biwa Marathon nchini Japan.

Simbu ambaye ni mshindi wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon ameonesha umahiri mkubwa katika mashindano hayo hasa ikizingatiwa kuwa mashindano hayo yalikuwa yanashirikisha vinara wengi wa riadha ulimwenguni wakiwemo Muethiopia Kenenisa Bekele  Wakenya Daniel Wanjiru, Bedan Karoki na Abel Kirui.

Mara baada ya ushindi huo salamu za pongezi zimekuwa zikimiminika huku Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande akisema kuwa kampuni yake imeridhishwa sana na ufanisi aliouonesha katika mashindano hayo. 

Alisema uwekezaji uliofanywa na kampuni hiyo katika kumdhamini Simbu umezaa matunda kwani kiwango cha mwanariadha huyo kimekuwa kikiimarika siku hadi siku.

 “Tumefurahishwa sana na kiwango alichoonyesha Simbu kwenye London Marathon. Hii ni ishara nzuri sana na tunaamini atafanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika jijini London Agosti  mwaka huu.”

Kwa upande wake, meneja wa mwanariadha huyo Francis John alisema kuwa ameridhishwa na kiwango alichoonesha Simbu na kwamba punde tu atakaporejea wataanza maandalizi kwa ajili ya ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yatakayofanyika Agosti mwaka huu.

Katika mashindano hayo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mkenya, Danie Wanjiru (2:05:48) akifuatiwa kwa karibu na Kenenisa Bekele (2:05:57) na Bedan Karoki.

Regards,

Shumbana.

No comments:

Post a Comment