Sunday 16 April 2017

Simbu kuanza safari ya kushiriki London Marathon


Na Mwandishi Wetu

MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu kesho Jumatatu atapanda pipa kwenda Afrika Kusini akiwa njiani kwenda Uingereza, ambako atashiriki London Marathon Jumapili ijayo Aprili 23.

Simbu anapitia Afrika Kusini kwa ajili ya kupatiwa viza ya dharura ya kuingia Uingereza baada ya kuikosa ile ya kawaida jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jana kuwa, Simbu ataondoka kesho Jumatatu kwenda Afrika kusini kushughulikia viza ya kuingia Uingereza kabla ya kwenda nchini humo ambako Jumapili atashiriki London Marathon.

Simbu alifuzu kwa mbio hizo baada ya kumaliza katika nafasi ya tano katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazil 2016 kabla ya kushinda mbio za Mumbai Marathon.

Kwa mujibu wa Gida, tayari mwanariadha huyo ameingia katika orodha ya wanariadha bora kabisa duniani na ndio maana waandaaji wa London Marathon kuna fedha atapewa mara tu atakapoanza mbio hizo (Appearance Fees).

Gidabuday alisema kuwa Simbu hata kama hatashinda mbio hizo lakini akimaliza tu amejihakikishia fungu nono na kama akimaliza, basi ataondoka na maelfu ya dola za Marekani.

Simbu endapo atashinda mbio hizo za London Marathon ataondoka na kitita cha dola za Marekani 55,000 kama zaidi yash Milioni 150, na kama atafanikiwa kuvunja rekodi ataongezewa dola za Marekani 25,000 (ikiwa ni zaidi ya sh Mil 50),

Mshindi wa kwanza hadi wa 12 wa mbio hizo ataondoka na kitita cha fedha, huku wale watakaokimbia muda bora bbila kujali kama umevunja rekodi ya njia au ya dunia, nao wataongezewa fedha za bonasi.

No comments:

Post a Comment